Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
          KIKOSI cha Azam FC kimeondoka Dar es Salaam leo mchana kwenda          Mtwara kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara          dhidi ya wenyeji Ndanda FC Jumamosi kwenye Uwanja wa Nangwanda          Sijaona mjini humo.
          Lakini katika kikosi hicho beki chipukizi Gardiel Michael na          washambuliaji wawili wa kigeni, Kipre Herman Tchetche wa Ivory          Coast na Ismaila Diara wa Mali hawamo.
          Meneja wa Azam FC, Jemadari Said amesema, Michael na Diara ni          majeruhi, wakati Kipre Tchetche hajarejea kutoka nchini kwao,          Ivory Coast alipokwenda kwa matatizo ya kifamilia.
          Kipre alikwenda kwao Ivory Coast baada ya mechi dhidi ya Mbeya          City mjini Mbeya wiki iliyopita na hakuwapo wakati timu hiyo          inafungwa 1-0 na JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini          Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
          Jemadari amesema wanakwenda Mtwara na kikosi kikubwa, kwa sababu          baada ya mchezo huo dhidi ya Ndanda, wanatarajiwa kwenda kucheza          mechi ya kirafiki dhidi ya Kariakoo United mjini Lindi.
          Mabingwa hao watetezi wanaofundishwa na kocha Mcameroon, Joseph          Marius Omog wana pointi 10 baada ya mechi tano, kati ya hizo          sare moja, wamefungwa moja na kushinda tatu.
          Azam FC inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu,          nyuma ya Mtibwa Sugar iliyopo kileleni kwa pointi zake 13 za          mechi tano pia, baada ya kushinda michezo minne na sare moja.
          Yanga SC iliyomaliza nyuma ya mabingwa Azam FC msimu uliopita,          pia wana pointi 10 baada ya sare moja, kufungwa moja na kushinda          mechi tatu, lakini wanakuwa nafasi ya tatu kwa kuzidiwa wastani          wa mabao.
Comments
Post a Comment