Tarehe 23 September 2011 kupitia blog yangu ya sanaa na muziki niliandika hivi… Bila wasiwasi ASLAY kutoka katika kampuni ya Mkubwa na Wanawe TMK, ana sauti yenye ukomavu kuzidi umri wake wa kimaisha ya muziki. Mwimbaji mzuri ni yule ambaye anapoimba we msikilizaji unapata hisia ya ujumbe anaoutuma. Aslay ananikumbusha sifa aliyokuwa akipewa Michael Jackson alipokuwa mdogo, alikuwa akiweza kuimba kwa hisia ambayo kwa kawaida hutokana na kupitia machungu au furaha unayoiimba. Nalisikia hilo katika sauti ya Aslay. Namuombea Mungu kijana huyu aepuke na ulevi wa aina yoyote ile ili aweze kufaidi kipaji hiki ambacho Mola amemjalia, kwani kwa sauti hii na management inayotakiwa hakuna ambacho hataweza kufanya. Mungu amjalie asidharau elimu ili aweze kutumia vizuri elimu yake kupata kila kinachostahili kutokana na kipaji chake. angalia hapa
Utabiri wangu unaonekana katika ujio wa YAMOTO BAND. Ni nani hawa YAMOTO?
UNAPUZUNGUMZIA Yamoto Band unakuwa umeshagusa majina ya vijana wanne ambao ni waimbaji wenye sauti tamu na vipaji vya hali ya juu, kutoka mikoa tofauti hapa nchini.
Nao si wengine bali ni kinara wao, Aslay Isihaka maarufu kwa jina la 'Dogo Aslay', Mbwana Yusuph Kilungi 'Maromboso', Enock Deogratius 'Enock Bella' pamoja na Bakari Abdul katuti 'Beka'.
Kwa sasa, vijana hao wamefanikiwa kuiteka vilivyo himaya ya muziki hapa nchini, ambapo macho na masikio ya mashabiki wengi yameelekezwa kwao na wakionekana kufuatiliwa kwa karibu zaidi.
Mwaka mmoja nyuma hakukuwa na Yamoto Band, kwa sababu bendi hiyo imeibuka miezi kadhaa iliyopita, huku chanzo chake kikiwa ni kibao 'Yamoto'.
Meneja wa TMK Wanaume Family, Said Fella anasema, uundwaji wa Yamoto band ulikuwa ni kama vile usiotarajiwa, kwa sababu walivyoanza walikuwa wakimchukua msanii mmoja mmoja mikoani walipokuwa wakifanya shoo.
"Mei 3, 2011, rafiki yangu aitwaye Idd alinikutanisha na mdogo wake ambaye ndiye Dogo Aslay, baada ya kumuona ana kipaji nikafanya naye shoo ya ZIFF mwaka huo, kabla sijamuingiza Studio kurekodi 'Nakusemea'," anasema Fella.
Fella anasema kuwa, nyimbo nyingine za Aslay baada ya kumchukua, ni 'Umbea Umbea' aliyoiachia mwaka 2012 ambayo alimshirikisha msanii Said Chigunda 'Chegge' na 'Bado Mdogo'.
Mwaka 2010, TMK walipozuru na kufanya maonesho mkoani Songea ndipo waliporudi na Enock Bella, aliyekuwa mnenguaji kijana anayetikisa mkoa huo.
Walipofika nae Dar es Salaam, wakamshauri ajifunze pia kuimba kwani unenguaji una mipaka yake kiumri tofauti na uimbaji, wakimtolea mfano wa Bi Kidude ambaye wakati huo alikuwa akiendelea kuonekana majukwaani licha ya kuwa na umri mkubwa.
"Jukumu la kumnoa Enock Bella nikamwachia Meneja wangu Chambuso, ambaye alimfundisha kuimba kwa kutumia gitaa na kinanda," anasema Fella.
Fella anasema kuwa, Desemba 2011, kama kawaida yao walizuru mkoani Morogoro, sehemu za Ifakara na kuibuka na kijana mwenye kipaji cha hali ya juu, ambaye si mwingine bali ni Beka.
Katika onesho walilolifanya Ifakara kwenye ziara hiyo, Beka alikuwa kati ya wasanii waliopiga shoo ya utangulizi, Fella akaonekana kuvutiwa naye, ambapo kabla hajamwambia chochote, Beka mwenyewe alimfuata na kumuomba kujiunga na kundi lake.
Alichokifanya Fella baada ya Beka kumuomba kujiunga na kundi la Mkubwa na Wanawe ni kumwachia nauli na kumwambia awafuate jijini Dar es Salaam atakapomaliza mtihani wake wa kidato cha nne.
"Maromboso, yeye alifika kwenye usaili wa wasanii, katika kundi la Mkubwa na Wanawe Oktoba 3, mwaka 2012, akiwa kidato cha pili," anasema Fella.
Wakapita wawili tu kwa kishindo kwenye usaili huo, yeye na kijana mwingine anayemkubuka kwa jina moja tu la 'Dick' akiwa kawakanyaga na kuwatupa huko wasanii wengine zaidi ya 25.
Fella anasema kuwa, baada ya hapo ndipo likaja wazo la kibao 'Yamoto' walichoshiriki kukiandaa vijana hao kwa ushirikiano mkubwa, wakakirekodi na kutokea kukubalika vilivyo.
Anasema kuwa, hadi sasa Yamoto Band wamefanikiwa kufanya mambo makubwa na kuwa miongoni mwa bendi zinazokubalika vilivyo kwa mashabiki ndani na nje ya Tanzania.
Akielezea malengo ndani ya Yamoto Band, Fella amekusudia kulifanya liwe linalotambulika kimataifa zaidi na kuzidi kuachia vibao vikali kwa faida ya mashabiki wao.
"Kwa upande wa kundi zima la Mkubwa na Wanawe, lina jumla ya wasanii 46 hadi sasa, wa fani mbalimbali za sanaa na utamaduni, zikiwamo muziki na maigizo," anasema Fella.
Fella anasema kuwa, bado anahitaji vijana wengine wengi wenye vipaji kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Temeke kujiunga na Mkubwa na Wanawe, ili kupunguza makali ya ajira kwa vijana.
Hivi sasa, Yamoto Band inatamba na vibao vitatu ambavyo ni 'Yamoto', 'Nitajuta' pamoja na 'Niseme' vinavyoonekana kushitua mioyo ya mashabiki hata wa miondoko mingine ya muziki.
Maskani ya yamoto Band kwa sasa ni Temeke, Mikoroshini ambapo ndipo ilipo Klabu ya kundi zima la Mkubwa na Wanawe.
Comments
Post a Comment