ASHA Bora nikweleze, jambo linalonikera kila siku,
ni tabia ya kumsifia, mchumba wako wa zamani,
mchumba huyo mmeachana, na sasa wewe ni wangu,
Asha kweli unaniudhi, kwa hakika unanisikitisha…."
Hicho ni kipande kidogo cha wimbo 'Asha Bora' wa DDC Mlimani Park Orchestra Sikinde, kilichorekodiwa katikati ya miaka ya 80, kikiwa kimebeba albamu yenye vibao 6, huku vingine badhi vikiwa ni 'Hapendeki', 'Halima' na 'Usia wa Babu'.
Kibao 'Asha Bora' chenyewe ambacho kimepangwa kiufundi ala na sauti, ni utunzi wa mcharazaji mahiri wa gitaa zito, Besi, Julius Mzeru.
Waliokuwa wanafuatilia vema muziki wa dansi wa kipindi kile, watakuwa wanalikumbuka vilivyo jina hilo la Mzeru, kutokana na kuwa, ameshiriki kucharaza Besi kwenye vibao vingi zaidi vya Sikinde.
Tamaa ya maisha mzuri zaidi na umaarufu, ndiyo iliyomfanya achomoke Sikinde mwaka 1995 na kuwaacha wenzie wakijiandaa kurekodi albamu iitwayo 'Maisha Mapambano'.
Aliondoka Sikinde pamoja na Salum Nyembo 'Kalamazoo', 'Henry Mkanyia, Tino masenge 'Arawa' na Gasper Kanuti, wakakabidhiwa vyombo vya muziki na mtu aliyemtaja kwa jina moja la Sewando, huyu aliwahi kuwa mwanamuziki wa bendi za sekondari ya Kwiro na Mkwawa High School Iringa.
Baada ya kumuongeza mpiga drums hatari, aliyewahi kutikisa kenye bendi ya Tancut Almas ya Iringa, Kejeli Mfaume, kulitosha kabisa kufanya waanzishe bendi iliyoitwa Tanzania Brothers, TZ Brothers.
Akiwa Tanzania Brothers, Mzeru alishiriki kurekodi albamu moja iliyokuwa na vibao kama 'Wazazi', 'Blandina', 'Maisha Magumu', 'Mama Kibiriti' na nyingine iliyopo katika miondoko ya Kingoni, ambayo ni utunzi wake.
Kuna mambo mengi mazuri yalianza kwa TZ Brothers, kama mkataba mnono Dodoma Hotel, kupiga muziki na wasanii wa kizungu na ziara ya nchini Uholanzi mwaka 2001, Mzelu aliitumikia Tanzania Brothers miaka sita, kuanzia mwaka 1995 hadi 2001 alipochomoka baada ya kurejea toka Uholanzi walipokaa na kutumbuiza kwa miezi miwili, sasa akaingia Tabora Jazz.
Mwaka 2005 aliamua kupanda boti hadi kisiwani Zanzibar, katika bendi ya Karafuu alipokutana na wakali kama Anania Ngolika na Eddo Sanga, akadumu hapo kwa miezi kadhaa tu akabwaga manyanga na kurejea jijini Dar es Salaam baada ya kukosana na Meneja wake wa bendi.
Safari hii alipotua Dar es Salaam, alikumbana na msoto mkali na kugeuka kuwa deiwaka kwenye bendi ya mtaani iliyokuwa ikiitwa Twiga, ambayo maskani yake yalikuwa Temeke, Dar es Salaam.
Mwaka 2007 alirudi tena Zanzibar lakini akiwa amekwenda kuanzisha kundi la Zaafro Band alilokaa nalo kwa muda wa mwaka mmoja akaikumbuka tena Dar es Salaam alipokuja Mtaa Hananasifu, Kinondoni kuasisi bendi ya Sweet Safari.
Sweet Safari nayo haikuwa na maisha marefu kwani ilisambaratika muda mfupi tu baada ya kuanzishwa kutokana na ubabaishaji na usaliti uliokuwa umewatapakaa wa baadhi ya wanamuziki.
"Kifo cha bendi ya Sweet Safari kilinipa wazo la sasa kuanza kufungua kundi langu, nikamfata mzee mmoja aitwaye Ibrahimu Didi ambaye ndiye mmiliki wa bendi ya Tabora Jazz, nikamuomba vyombo," anasema Mzeru.
Mzeru anasema kuwa, Didi alimkabidhi vyombo lakini kwa sharti kuwa bendi atakayoianzisha lazima iitwe 'Tabora Matata', naye hakuwa na jinsi kukubali kwavile alikuwa amekwama.
Mzeru anyemtaaja mmiliki wa bendi ya WK Sound, 'Kagusa' kuwa sehemu ya msaada alipokuwa Tabora Matata, kwa sababu alikuwa akijitolea kumnunulia baadhi ya vifaa kila vilipoharibika au kukosekana kabisa.
Alifanya maonesho kwa muda wa mwaka mmoja akitumia jina la 'Tabora Matata', huku akijinyinyima na kununua vyombo vya kwake kidogokidogo ambapo mwaka 2010 alianza kuvitumia huku akishirikiana na Kagusa.
Hatimaye, mwaka 2011 alifuta kabisa utumwa wa kushirikiana na mtu mwingine kwenye vyombo baada ya kukamilisha vya kwake na bendi yake kuiita JM Mbeta.
Mzeru mwenye mkakati wa kuitangaza JM Mbeta kimataifa, anasema anajisikia faraja zaidi wakati huu anapotumia vyombo vyake mwenyewe, hata kama kipato chake si cha kuridhisha.
JM Mbeta inatamba na vibao vyake kadha ambavyo hata hivyo bado havijarekodiwa, navyo ni 'Mke wangu kajinyonga', 'Chelewa Chelewa' na 'Unanionea Bure', 'Ni Wewe Uliyenikosea', 'Monica' na 'Siku Nyingi Nakuwaza'.
Ukimuondoa Mzeru mwenyewe anayecharaza gitaa la Solo, wanamuziki wengine wanaounda bendi hiyo wote ni watoto wake; Charles Mzeru, Fred Mzeru, Jacob Mzeru, Joel na Mzeru Machine.
Bendi yake ya kwanza kuitumikia ilikuwa ni Los Tazal aliyojiunga nayo mwaka 1972, kabla ya makundi mengine mbalimbali yakiwamo Orchestra Continental, Lumaliza Jazz na National Panasonic.
Unapomuuliza namna alivyoingia Sikinde, Mzeru anakujibu kuwa, alijiunga nao mwaka 1982 baada ya Hassan Bitchuka na Joseph Mulenga kwenda kurekodi Kenya katika bendi ya Black Worries.
Aliingia kama mcharazaji gitaa la Solo lakini baadaye ilibidi amsaidie marehemu Suleiman Mwanyiro aliyekuwa peke yake katika besi na kibao chake cha kwanza kurekodi ni 'Edita'.
Tukio kubwa analolikumbuka Mzeru anayejivunia uzoefu katika muziki, maisha bora na kumiliki bendi yake, ni kazi kubwa aliyoifanya Sikinde hata mwaka 1984 kutokea kuwa mfanyakazi bora shirika zima la DDC.
"Nilianza muziki tangu nikiwa na umri wa miaka 10, kwa kutengeneza magitaa ya makopo, baada ya kuvutwa na wanamuziki nguli wa enzi hizo kama Papa Noel, James Brown, Franco na Dk. Nicco Kasanda," anasema Mzeru.
Alisoma shule ya msingi Tandika, kuanzia mwaka 1963 hadi 69 na kujiendeleza na masomo mengine madogomadogo na kufanyakazi kwenye kiwanda cha blanketi kwa miaka saba.
Ni baba wa familia mwenye mke na watoto saba, ambao ni Veneranda, Suzana, Charles, Fred na Joel.
Comments
Post a Comment