TUMEANGUKA KWA MARA YA PILI, LAKINI NADHANI BADO HATUJAKATA TAMAA”-NAHODHA JOSEPH OWINO





TUMEANGUKA KWA MARA YA PILI, LAKINI NADHANI BADO HATUJAKATA TAMAA"-NAHODHA JOSEPH OWINO
Owino ni beki tegemeo katika safu ya ulinzi ya Simba sc
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
NAHODHA wa Simba, Mganda, Joseph Owino amesema wachezaji wa klabu hiyo hawajakata tamaa kwa matokeo waliyopata katika mechi mbili za ligi kuu soka Tanzania bara.
Simba ilitoka sare ya 1-1 na Polisi Morogoro katika mechi ya raundi ya pili ya ligi kuu iliyopigwa jana uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Katika dakika ya 32 , Emmanuel Okwi aliifungia Simba bao la kuongoza akimalizia pasi ndefu ya Mohamed Hussein 'Tshabalala' kutoka upande wa kushoto wa uwanja, huku mabeki wawili wa Polisi akiwemo Lulanga Mapunda wakimuacha Mganda huyo atulize mpira kifuani katika eneo la hatari na kutikisa nyavu.

Katika dakika 50 Danny David Mrwanda alifunga goli la kusawazisha baada ya mabeki wawili wa Simba, Masoud Nassor 'Cholo' na nahodha Joseph Owino kugongana na kumuacha nyota huyo wa zamani wa Simba akifunga.
Kabla ya mechi hiyo, Septemba 20 mwaka huu, Mnyama aliambulia sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union katika mechi ya ufunguzi wa ligi kuu uwanja huo huo wa Taifa.
Kipa wa Polisi Morogoro, Abdul Ibad akijaribu kuokoa bila mafanikio mpira ulipigwa na Okwi na hatimaye Simba kuandika bao la kuongoza


Baada ya matokeo hayo, Owino alisema: "Tumeanguka kwa mara ya pili, lakini nadhani bado hatujakata tamaa. Tutaendelea kujituma zaidi mpaka tupate ushindi".
"Hakuna makosa, sababu ni kwamba ligi ndio inaanza, timu zinashindana kupata pointi, lakini tunajipanga kufanya vizuri'.
Simba walianza mechi kwa kutawala safu ya kiungo ambapo Jonas Mkude alionesha kiwango kizuri. Alitawala dimba la kati, alikuwa na jeuri, alipiga pasi sahihi na kuipandisha timu juu, lakini mambo yalibadilika kipindi cha pili.
Mkude alionekana kuchoka, wakati huo huo Piere Kwizera, Shaaban Kisiga, Emmanuel Okwi waliokuwa mbele yake walishindwa kurudi nyuma ipasavyo na kuisaidia timu.
Kuhusu safu ya kiungo, Owino amekiri kwamba haifanyi vizuri, lakini anaamini kocha Patrick Phiri atafanya kazi.
Owino alisema: "Safu ya kiungo haichezi vizuri sana, lakini mwalimu atafanyia marekebisha na tutacheza vizuri zaidi".

Wekundu wa Msimbazi watacheza mechi ya raundi ya tatu Oktoba 4 mwaka huu uwanja wa Taifa dhidi ya Stand United.


Comments