TANAPA, MAMLAKA YA NGORONGORO NA SHIRIKA LA NDEGE LA ETHIOPIA WADHAMINI WAKUU ‘SWAHILI INTERNATIOANL TOURISM EXPO’



TANAPA, MAMLAKA YA NGORONGORO NA SHIRIKA LA NDEGE LA ETHIOPIA WADHAMINI WAKUU 'SWAHILI INTERNATIOANL TOURISM EXPO'
 Na: Geofrey Tengeneza

Shirika la hifadhi la taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro pamoja na shirika la ndege la Ethiopia wamedhamini onesho la kimataifa ya utalii lijulikanalo kama 'Swahili International Tourism Expo' (S! TE).

Taasisi hizo tatu zinakuwa ndio wadhamini wakuu wa maonesho hayo ya kimataifa ya utalii ya kwanza Tanzania yanayoandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Pure Grit Project and Exhibition Management Ltd ya Afrika Kusini ambao pia ndio waandaji wa onesho la utalii la INDABA linalofanyika kila mwaka Afrika Kusini.. Onesho hili la kwanza la S!TE litafanyika kuanzia mwezi Oktoba, tarehe 1 – 4, 2014 katika ukumbi wa mikutano Mlimani City. Pamoja na maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali za utalii lakini pia kutakuwa na maonesho ya utalii wa utamaduni wa mtanzania.


Aidha sambamba na maonesho kutakuwa pia na kongamano kwa muda wa siku zote nne ambapo mada mbalimbali kuhusu utalii zitawasilishwa na wataalamu katika sekta ya utalii na kujadiliwa.


Onesho hili la utalii la kimataifa ambalo lmelenga watalii wanaokuja Afrika yanatarajia kuvuta maelfu ya wasafirishaji wakubwa wa watalii na wadau wa sekta ya kitalii na usafiri kutoka kila pande za Dunia. Kama sehemu ya udhamini wake, licha ya mashirika mengine, shirika la ndege la Ethiopia ndilo litakuwa wasafirishaji wakubwa wa watalii na wandishi wa habari wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali duniani zikiwemo Marekani, Uingerza, Ujerumani n.k wanaokuja kwa ajili ya onesho hili.

S!TE litakalo kuwa likifanyika kila mwaka mwezi Oktoba, litachukua muundo wa maonesho ya kiusafiri na kibiashara likilenga pia katika kuonyesha utalii endelevu wa kisasa, uhifadhi na mambo mengine yanayohusiana na masoko ya utalii.


Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania imebeba vivutio mbalimbali vya kitalii kama vile mlima Kilimanjaro, Zanzibar na hifadhi ya Taifa ya Serengeti.


Kwa ujumla Tanzania inaweza tu kuitwa kitovu cha vivutio vya asili Afrika kwani Tanzania ndio nchi pekee yenye vivutio vitatu kati ya saba vya asili barani afrika ambavyo ni Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote barani afrika; Ngorongoro Crater ambayo ni kubwa duniani isiyomomonyoka, na hifadi ya Taifa ya Serengeti, maarufu kwa nyumbu wanaohama wakiwa katika makundi makubwa na misururu mirefu kutoka kusini kuelekea kaskazini na kurejea.


Comments