SOMA VALANGATI LA MKUTANO WA SHIRIKISHO LA MUZIKI NA MAPICHA KIBAO



SOMA VALANGATI LA MKUTANO WA SHIRIKISHO LA MUZIKI NA MAPICHA KIBAO

Mkutano ulioitishwa na Baraza la Sanaa la Taifa kuzungumzia mstakhabari wa tasnia ya muziki, umeishia kwa zogo kubwa lililosababisha umalizike kwa kutolewa ahadi na Mwenyekiti wa Mkutano huo Kaimu Katibu Mkuu wa BASATA Bwana Godfrey Ngereza ya kuitisha mkutano wenye wajumbe tofauti. Mapema kabisa wakati baada ya utambulisho wa waliohudhuria kulianza kuonyesha tatizo kwani mmoja kati ya Marais wawili wa Shirikisho hilo wanaopingana,  Bi Stara Thomas kudai kuwa mkutano huo una wajumbe ambao hawastahili kuwemo kutokana na Katiba ya Shirikisho. Hili lilipelekea kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanamuziki, John Kitime kuulizia kuhusu hali ya mkutano. Binafsi alisema aliitwa kenye kikao na BASATA kwa hiyo swala la Katiba linamchanganya, kwani kama ni wito wa BASATA kila msanii anakuwa na haki sawa kuchangia , lakini kama ni kikao cha Shirikisho ieleweke ili kuleta muafaka. Hatimae ikaonekana kuwa wasemaji watakuwa viongozi wanaogombania madaraka na wajumbe wengine kuwa wasikilizaji tu.

Bi Stara Thomas mmoja wa Marais wawili akaanza kuelezea anavyofahamu hali ilivyo na kilichopelekea yeye kuteuliwa kuwa Rais wa muda wa Shirikisho. Kubwa lilikiwa na shilingi 900,000/- ambazo zilichangwa kwa ajili ya rambirambi kwa mke wa Marehemu Gurumo, ambapo Bi Stara alisema Katibu wake Mkuu, Bwana Kaswahili alimtaarifu kuwa Rais aliyekuwa madarakani Bwana Addo November Mwasongwe alikula fedha hizo, hivyo kupelekea Kamati yote ya uongozi wakati huo kuondolewa madarakani kwa kikao kilichoitishwa na Katibu Msaidizi wa muda Francis Kaswahili, na kumsimika Bi Stara kuwa Rais.

Hatimae Addo alipewa nafasi ajieleze ambapo alikiri kupokea fedha hizo na kuongeza nyingine laki mbili kama mchango binafsi na kufanya ziwe milioni moja na laki moja, ambazo yeye na wajumbe wengine wa uongozi wake waliona ni busara kumpatia mke wa marehemu mara baada ya yeye kumaliza eda. Kabla hilo halijafanyika, Francis Kaswahili alikuja na mtoto wa marehemu na kudai kuwa fedha hizo apewe mtoto wa marehemu, jambo ambalo lilipingwa kwani mke wa marehemu ndie alikuwa akiisha marehemu toka ndoa yao 1968, na ndie aliyemtunza marehemu mpaka umauti wake. Bwana Addo alisema kulikuweko na makubaliano kati ya mke wa marehemu na viongozi chini ya Addo kutafuta michango na kuongeza fedha hizo mpaka ziweze kununua Bajaj na mama akabidhiwe Bajaj ili iwe kitega uchumi cha kuweza kumfanya aishi. Na kwa maelezo ya Addo ni kiasi kidogo tu kimebaki kabla ya kuweza kukamilisha fedha ya kununua kibajaji hicho. Kabla Addo hajamaliza Stara alijaribu kuingilia kati jambo ambalo liliamsha hisia za wajumbe na kumtaka afuate taratibu katika kutoa hoja zake kwani ilipokuwa zamu yake kuzungumza hakuna aliye mkatisha.

Wakati ubishi huu ukiendelea ghafla ilitolewa taarifa kuwa kuna mtu kasema, 'DAMU LAZIMA IMWAGIKE" hili lilileta zogo jingine ambalo hatimae lilitulizwa. Kisha  Francis Kaswahili ambaye ndie aliyejitwalia cheo cha Katibu Mkuu wa Shirikisho alianza kusoma ripoti ya hali ya chama, lakini lugha yake ikaonekana kuwa inawakera baadhi ya wanamuziki wa muziki wa Enjili waliokuwepo pale nao kuanza kupiga kelele kuwa hawamtaki. Vurugu hizi hatimae zilimfanya Kitime aingilie kati na kumuomba Katibu Mtendaji wa BASATA aahirishe kikao na kukifanya katika mfumo tofauti hali iliyowezekana na kikao kikaahirishwa na kuacha wanamuziki wakizagaa maeneo ya BASATA katika vikundi wakielezana hili na lile kutokana na yaliyojiri.IMG_0028 IMG_0019 IMG_0034 IMG_0041 IMG_0046 IMG_0048 IMG_0049 IMG_0051



Comments