
Salum Abdallah
Salum Abdallah Yazidu-SAY

Kushoto-Kibwana Seif, kulia Salum Abdallah.
Cuban Marimba Band
Morogoro ni moja ya miji iliyokuwa maarufu kwa burudani katika miaka ya 1950, 1960 na 1970. Watu walitoka Dar es Salaam na kufuata week end Morogoro. Hali yake ya hewa, na kuwepo kwa bendi mbili kubwa maarufu zilizokuwa na uwezo mkubwa zilifanya wafanyakazi watake kupangwa kituo cha Morogoro. Kati ya hizo bendi mbili, ilikuweko Cuban Marimba Band. Bendi hii ilikuwa ndoto ya mwanamuziki Salum Abdallah Yazidu, maarufu kama SAY. Salum Abdallah alizaliwa tarehe 5 Mei, mwaka 1928. Baba yake alikuwa mwarabu na mama yake Mlugulu mwenyeji wa Morogoro. Alisoma mpaka darasa la sita pale Msamvu na akachaguliwa kuendelea na shule Dar es Salaam, maana wakati ule ililazimika kuja Dar es Salaam ili kuendelea na masomo baada ya hapo. Pamoja na kufaulu huko baba yake aliamua abakie nyumbani kumsaidia katika shughuli za biashara. Katika kipindi hiki Salum alianza kuonyesha kupenda kwake muziki. Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa maarufu kwa kuitwa kwa namba zake. Gv1, GV2, GV3 na kadhalika. Pamoja na baba yake kutokupenda aina ya muziki aliokuwa anaupenda mwanawe, aliona ni heri amnunulie gramafon ya kupigia hizo santuri ili atulie. Haukupita muda mrefu Salum alitoroka kwao ili aende Cuba kujifunza muziki. Alitoroka hadi Mombasa ili apande meli kwenda Cuba, ilikuwa mwaka 1945 kulikuwa bado na vuguvugu la vita ya pili ya dunia na safari yake ikaishia Mombasa. Alipata matatizo pia Mombasa na kuibiwa fedha zake na kulazimika kuanza kuchoma mishkaki huko. Umoja wa Waarabu wa Mombasa wakamtaarifu baba yake ambaye hatimae alimrudisha Morogoro, kisha akamfungulia mgahawa ili atulie , lakini Salumu alikuwa kishapata mzuka wa muziki na akawa ameanza kuhudhuria madansi na kupendezwa sana na vifaa vya Dar Es Salaam Jazz Band, wakati huo yeye na wenzie walikuwa wameanzisha kikundi ambacho kilikuwa na vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili wenyewe wakikiita bendi na kuipa jina, La Paloma, hili lilikuwa jina la wimbo mmoja katika santuri za GV, nyimbo hii ni nzuri kiasi cha kwamba mpaka leo bado inapigwa duniani kote, na hata kurekodiwa na wanamuziki mbalimbali akiwemo Elvis Presley aliyeingia katika anga za muziki baadae sana. La Paloma , ilikuwa na viongozi kama Juma Said-Rais ,Abubakar Hussein- Mweka hazina, Ramadhan Salum-Katibu Mkuu, Ali Waziri –Naibu Katibu Mkuu na Salum Abdallah mwenyewe akiwa Band Master.
Katika kuiona Dar Es Salaam Jazz Band, hamu ya kuwa na vyombo kama vya Dar Jazz ilikuwa kubwa kiasi cha Salum kuuza kwa siri nyumba moja wapo ya baba yake na kununua vyombo kama vya Dar Es Salaam Jazz band. Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi rasmi. Viongozi wake walikuwa Salum Abdallah-Kiongozi, Abubakar Hussein-Mweka Hazina, Juma Ndehele-Katibu, wanamuziki walikuwa Kibwana Seif, Juma Kilaza, Ligongo,Mgembe,Juma Kondo,Nzige, Daulinge. Kundi hili mwaka 1952 likajipa jina la Cuban Marimba Jazz Band. Kundi lilianza kuwa maarufu kiasi cha kuwa mwaka huohuo kampuni ya santuri ya Mzuri Records walikuja mpaka Morogoro kurekodi nyimbo za bendi hii. Bendi iliendelea na umaarufu mkubwa mpaka kwenye miaka ya 70. Salum Abdallah alifariki katika ajali ya gari, ambapo taa za gari lake zilizimika ghafla akiwa katika mwendo na gari lake likatoka nje ya barabara na kumtupa nje akapasuka kibofu na kufariki siku hiyo. Ilikuwa tarehe 19 Novemba 1965.
(Picha kwa hisani ya Jumaa R. R. Mkabarah)
Comments
Post a Comment