NEW VICTORIA SOUND KARIBUNI SANA SOKONI, LAKINI MNA LIPI JIPYA?



NEW VICTORIA SOUND KARIBUNI SANA SOKONI, LAKINI MNA LIPI JIPYA?
NEW VICTORIA SOUND KARIBUNI SANA SOKONI, LAKINI MNA LIPI            JIPYA?

JUMAMOSI ya tarehe 4 Octoba mwaka huu, bendi iliyosukwa upya Victoria Sound itatambulishwa rasmi kwa mashabiki wa muziki pale New Msasani Club.

Japo Victoria Sound inatambulishwa upya, lakini bendi hii si ngeni sana maskioni mwa mashabiki, ina umri mrefu tu – ipo ulingoni kwa zaidi ya miaka sita. Jina Victoria Sound lilianza kutumika mwaka 2007.

Na hata kabla ya kuitwa Victoria Sound, bendi hii ilikuwepo kwa miaka mingi huku nyuma ikitumia majina kadhaa yakiwemo VB Sound, City Sound na City Victoria. Kwahiyo ukichimba kwa undani chimbuko la bendi hii, utangundua ina umri wa zaidi ya miaka 20.

Wanamuziki kadhaa wenye majina makubwa kama vile Mobali Jumbe, Mensah Abdallah, Rajab Niva, Ally Moshi, Haruna Lwale na John Kijiko wanaingia katika historia ya wasanii waliowahi kuitumikia bendi hii, achilia mbali ujio wa Mwinjuma Muumin na Waziri Sonyo.

Victoria Sound haikuwahi kufanya maonyesho ya kutegemea kiingilio hadi pale Mwinjuma Muumin alipojiunga nayo mwaka jana ambapo alijaribu kutengeneza vibao kadhaa vikiwemo "Shamba la Bibi" vilivyoifanya bendi hiyo ianze kupata umaarufu ikiwa ni pamoja na kufanya maonyesho kadhaa ya kutegemea kiingilio cha mlangoni.

Lakini haikuchukua muda mrefu, bendi ikaanza kusinzia, Muumin akaondoka, Waziri Sonyo naye akatimka – bendi ikarejea kwenye maisha ya kutegemea show za kiingilio 'kinywaji chako'.

Bendi hii sasa imesukwa upya na itatambulika kama New Victoria Sound.

Imekusanya nyota kadhaa kutoka Msondo Ngoma na Sikinde wakiwemo mpuliza saxophone Shaaban Lendi, Edo Sanga,  Adolph Mbinga, James Mawila na Karama Legesu.

Maswali ya msingi kwa Victoria Sound ni haya yafuatayo: Je wana jipya gani? Wamejipangaje? Wanamuziki wapya wana tiba gani itakayowatofautisha na vizazi vingine vya bendi hiyo ambavyo havikuweza kuifanya iwe moja ya bendi bora hapa nchini?

Kuchukua nyota wa Msondo au Sikinde si suluhisho. Kuongeza neno "New" kwenye jina lao si suluhisho. Kuizindua upya bendi yao pia si suhisho.

Muziki wa dansi umeporokoma, soko la muziki wa dansi limejaa, kumbi zenye neema kwa bendi za dansi nazo zimetoweka. Takwimu zinaonyesha wazi kuwa kila zinapoanzishwa bendi mpya tano, basi nne  au zote hufa kifo cha kawaida.

Kwa namna soko lilivyo, ili bendi mpya ifanikiwe basi ni lazima bendi kadhaa za zamani ziporomoke – wateja ni wale wale hivyo njia pekee ya kuishi ni kunyang'anyana hao wateja wachache waliopo.

Hakuna ubishi kuwa maisha mazuri ya bendi mpya huwa ni pale bendi inapokuwa kambini. Hapa kila kitu huwa ni swafi. Hapa ndipo tajiri wa bendi anaweza kufanya lolote mtakalohitaji – kuanzia promo, posho za uhakika, usajili wa wasanii nyota. Hili ndilo eneo ambalo msanii anaweza kudeka vile atakavyo.

Lakini pale bendi inapoanza rasmi kazi, basi ndipo mbivu na mbichi hujulikana, ugumu wa soko hujulikana hapo, hasara au faida kwa mwenye bendi hujulikana hapo, majuto au furaha ya ushindi huja hapo, uswahiba au kukwepana kwa wanamuziki na bosi wao huanzia hapo. Kwa kifupi biashara ya kumiliki bendi ni pasua kichwa, inabidi ujipange kisawasawa.

New Victoria Sound lazima waje na tungo za kipekee, muziki wa kipekee – muziki utakaowatofautisha kwa sana tu na bendi zingine. Wakipita mle mle zinakopita bendi zilizopo basi wajiandae kuendelea na show za kiingilio kinywaji chako. Kwa leo ni hayo tu, tukutane tena Jumatatu ijayo.



Comments