FILAMU mpya ya muimbaji wa nyimbo za Injili, Jennifer Mgendi iitwayo 'Mama Mkwe' inatarajiwa kuigizwa sokoni siku ya Alhamisi baada ya kukwama kuachiwa jana Jumatatu kama ilivyokuwa imepangwa.
Aidha Muinjilisti huyo amewataka mashabiki wake wasiikose kupata darasa la kutosha.
Jennifer alisema filamu hiyo itaachiwa rasmi Septemba 25 baada ya jana kukwama kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake ikiwa ni wiki kadhaa tangu kumalizika kurekodiwa kwake na kusema kwa ujumbe uliopo ndani yake, mashabiki hawapaswi kuikosa.
Muimbaji huyo alisema, kisa cha Mama anayeingilia ndoa ya mwanae wa kiume akitaka kupatiwa mjukuu ni mambo ambayo yamekuwa yakiwakumba wanajamii wengi na kusambaratisha ndoa zao bila kutaka.
"Ni mambo yanayotokea ndaniya jamii na kuwaachia watu machungu, sasa waigizaji wameonyesha uhalisia wa mambo namna ndoa nyingi zinavyosambaratika kwa sababu ya mambo kama hayo," alisema.
Katika filamu hiyo, Jennifer ameigiza na wasanii wengine wakali kama kina Mussa Banzi, Bahati Bukuku, Christine Matai, Bibi Esther na wengine.
"Itakuwa mtaani Alhamisi, mashabiki wasikose kuona uhondo huu. Mama Mkwe ni zaidi ya kazi zangu za nyuma kwa namna ilivyosukwa na kutendewa haki na wasanii walioigiza," alitamba Jennifer.
Comments
Post a Comment