MJUE MSANII WA FILAMU, LOMOLE MATOVOLWA ‘BIGGIE’


MJUE MSANII WA FILAMU, LOMOLE MATOVOLWA 'BIGGIE'

Big

"NILIANZA kucheza maigizo tangu mwanzoni mwa miaka ya 80, nikiwa darasa la pili, kwa kuigiza katika matukio mbalimbali ya kishule kama vile mahafari," hivyo ndivyo anavyoanza kujielezea Lomole Matovolwa 'Big', mmoja kati ya wasanii mahiri wa filamu za Kibongo. 

Kutokana na uhodari wake wa kucheza filamu na michezo ya kuigiza ya jukwaani, Big aliyewahi kushiriki muvi kama vile; 'Masaa 24', 'Binti Nusa', 'Mahabuba' na 'Love is War' na nyinginezo nyingi, amejikuta akijikusanyia mashabiki na wapenzi kemkem. 

Katika mazungumzo yake na mwandishi wa makala hii, Big anasema mara nyingi aliigiza kama baba wa familia kutokana na umbo lake, ambapo baadhi ya waliokuwa wakimuona walitabiri atakuja kuwa tishio baadaye.

 Mwaka 1999, kwa mara ya kwanza, alijiunga na kundi la maigizo lililokuwa likijulikana kwa jina la 'Mwana Arts Group' ambalo maskani yake yalikuwa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, ambako alishiriki kikamilifu katika michezo hii na ile ya jukwaani.

 Mwaka 2001 alilipa kisogo kundi hilo na kujiunga na kundi lingine la 'Nyota Academia' alikokutana na waigizaji wakali wanaoendelea kutamba hadi sasa katika filamu, kama vile; Single Mtambalike 'Rich Richie', Jacob Stephen 'JB', Yvonne Cherrie 'Monalisa' na Haji Adam 'Baba Haji'.

 "Nikiwa na kundi hilo la Nyota Academia, kwa nyakati tofauti nilishiriki kucheza michezo mingi tu ya kuigiza katika runinga za CTN na CTN Clouds, ambapo miongoni mwa michezo hiyo ni ile iliyotokea kutikisa vilivyo ya 'Wimbi' na 'Kamanda'," anasema Big.
 
Mwaka 2004, alichomoka Nyota Academia na kuwa mmoja wa waanzilishi wa kundi la 'Kamanda Family' analolisifu kuwa lilifanya vema mno katika runinga ya TBC1 (wakati huo ikiitwa TVT) kwa kuigiza Tamthiliya za 'Jirani' na Uhondo wa Ngoma'.

 Big, mwenye uzito wa kilo 120 hivi sasa, anakumbuka kuwa, mwaka 2006 alishiriki Tamasha la filamu la nchi za Majahazi (ZIFF), lililofanyika kisiwani Unguja alikoshiriki kucheza Tamthilia ya jukwaani inayokwenda kwa jina la 'Mfalme Juha'.

Mwaka 2007, alishiriki kumuigiza nduli Idd Amin Dadah, katika igizo la jukwaani lililoitwa 'Juliana' ambalo lilifanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

 "Katika onyesho hilo, mgeni rasmi alikuwa mke wa Rais, Mama Salma Kikwete ambaye alifurahia kuona kuwa, nimemudu vilivyo kumuigiza Nduli, kiasi cha kuamua kupiga picha ya kumbukumbu na mimi," anasema Big. 

Baada ya onyesho hilo lililomuingizia pesa nyingi kuliko kazi yoyote aliyowahi kuifanya, mwaka 2008, alifungua Kampuni yake binafsi aliyoamua kuiita 'Kula Kulala Entertainment and Film Production' ambayo sasa ameibadilisha jina na kuiita 'L.A Creative'.
 
Akiwa na Kampuni yake hiyo ambayo maskani yake yake yapo Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, tayari ameshatoa kazi mbili moto wa kuote ambali; 'Fundo la Roho' na 'Tozi' ambayo ni ya vichekesho.
Hivi sasa yuko katika maandalizi ya muvi yake mpya iitwayo 'Alhamdulillah' aliyowashirikisha wasanii chipukizi watupu ambao hata hivyo, ni wenye uwezo mkubwa kiuigizaji.
Kabla ya 'Alhamdulillah', Big alishatoa muvi iitwayo 'Mtihani' iliyochezwa na mastaa wengi wakiwamo Thabit Abdul, Belinda pamoja na Elizabeth Chijumba 'Nikita'.

Akiizungumzia zaidi filamu hiyo ya 'Alhamdulillah', Big anasema kuwa, anaamini itakuwa  zaidi ya filamu nyingine zote alizowahi kucheza, hasa kutokana na kuiandaa kwa utulivu mkubwa na kwa muda mrefu zaidi wakitumia vifaa vya kisasa katika uchukuaji picha.

 Kwa upande wa matarajio, Biggie asiyependa majungu na kukwamishana kimaisha, analenga kuwa mwigizaji bora zaidi atakayetambulika hadi nje ya bara la Afrika, ambapo atakuwa katika nafasi nzuri ya kuitangaza nchi yake anayodai kuwa anaipenda sana.

 Huyo ndiye Lomole Matovolwa 'Biggie',  aliyezaliwa katikati ya miaka ya 1970 na kubahatika kupata elimu yake ya msingi katika shule tatu tofauti za Mwongozo jijini Dar es Salaam, Holili, Rombo na Kia, Moshi mkoani Kilimanjaro.

"Elimu ya sekondari niliipata katika shule ya Kolila iliyoko Old Moshi, mkoani Kilimanjaro na kumalizia Kilimanjaro Technical and Commercial Training Centre za mkoani Kilimanjaro," anasema Big.
 
Mwaka 1998, alijiunga na kozi masomo ya makenika, katika chuo cha ufundi VETA jijini Dar es Salaam, kabla ya kusomea Ubaharia katika chuo cha Darmarine. 

Hivi sasa Biggie ambaye ni baba wa familia mwenye mke Fatma Faraji Matovolwa na mtoto mmoja wa kike aitwaye Talhia, anaishi nyumbani kwake Mwananyamala Dar es Salaam.



Comments