Fahad                Musana, ambaye ni shabiki wa kutupwa wa klabu ya soka ya                Chelsea, amefariki dunia baada ya mchezaji wa zamani wa                klabu hiyo, Frank lampard, kuifungia Manchester City bao                la kusawazisha, katika pambano lililopigwa jana baina ya                timu hizo mbili.
        Musana, mwenye umri wa              miaka 24, na ambaye alikuwa mcheza kandanda la kulipwa              nchini Uganda, alikuwa akitizama mechi hiyo iliyovuta hisia              za mashabiki wengi katika kona mbalimbali za dunia, na              alianguka na kuzimia mara baada ya Lampard kusawazisha bao,              ikiwa ni dakika chache sana tangu aingie kutokea benchi,              katika dakika za lala salama.
        Alithibitishwa kuwa              amefariki baada ya kuwasili katika hospitali ya kijeshi ya              Bombo, na rafiki wa karibu wa marehemu amenukuliwa na vyombo              vya habari akisema "Jamaa, amekuwa ni shabiki wa kweli wa              Chelsea, ambaye angeweza kufanya lolote lile kwa ajili ya              klabu hiyo. Tulifanya naye mazoezi asubuhi ya jumapili, na              hata mchana tukala chakula cha mchana pamoja, hakika              inasikitisha"
        Tukio hili la kusikitisha,              limethibitishwa na Shirikisho la vyama vya soka nchini              Uganda (FUFA), ambalo limetoa tamko lake kufuatia mkasa huu              wa kushtusha.
        "FUFA, limekumbwa na              mshtuko baada ya kupokea taarifa za kifo cha ghafla cha              mchezaji wa klabu ya Simba ya Uganda, Misana Fahad, katika              hospitali ya Bombo. Mwili wa marehemu bado uko hospitalini              hapo, na taratibu za mazishi zinaandaliwa na taarifa              zitatolewa baadae", sehemu ya taarifa ya FUFA imesomeka              hivyo.
        Hii si mara ya kwanza kwa              mashabiki wa soka kufariki kufuatia timu wanazozishabikia              kushindwa kuibuka na ushindi katika mechi zao. Kumbukumbu za              hivi karibuni sana kwa ukanda wetu wa Afrika Mashariki na              Kati, ni za shabiki mwingine wa soka aliyefariki dunia msimu              uliopita, baada ya timu aliyokuwa akiishabikia ya Manchester              United kupoteza moja ya mapambano yake, ilipokuwa chini ya              kocha David Moyes
        
Comments
Post a Comment