MANCHESTER United wamewaduwaza watu wengi baada ya kuongoza 3-1 dhidi ya timu dhaifu iliyopanda daraja msimu huu Leicester City, lakini mwisho wa siku ikaambulia kipigo kikubwa cha bao 5-3.
Robin van Perisie aliipatia United bao la kuongoza dakika ya 12 kabla ya Angel Di Maria kutupia la pili dakika ya 16 na kutoa picha kuwa mabingwa hao wa zamani wataibuka na karamu nzito ya magoli.
Ukuta wa Manchester United umeonyesha udhaifu mkubwa baada ya kuruhusu magoli kuingia kiulani ambapo dakika ya 18 Jose Leonardo Ulloa akaipatia Leicester City bao la kwanza na kufanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa 2-1.
Manchester United iliyokuwa ugenini, ikafunga bao la tatu dakika ya 57 kupitia kwa kiungo Ander Herrera na huo ukawa ndio mwisho wao wa kugusa nyavu za Leicester City ambayo ilipata bao lake la pili kwa njia ya penalti katika dakika ya 62 mfungaji akiwa David Nugent.
Leicester wakapiga bao la kusawazisha kunako dakika ya 64 kwa bao la Esteban Cambiasso, Jamie Vardy akapachika la nne katika dakika ya 79.
Beki chipukizi Tyler Blackett akazawadiwa kadi nyekundu baada ya kufanya faulo iliyosababisha penalti iliyopigwa vema na Jose Leonardo Ulloa na kuzaa bao la tano dakika ya 83.
Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya England, Tottenham Hotspur ikiwa nyumbani kwake imepigwa bao 1-0 na West Bromwich Albion, bao lililofungwa na James Morrison dakika ya 74.
Comments
Post a Comment