MABAO MATAMU YA FREE KICK YANOGESHA MECHI YA SIMBA NA COASTAL UNION …Wekundu wa Msimbazi watangulia 2-0 lakini Wagosi wa kaya wakachomoa zote
DAKIKA ya nne, kiungo mshambuliaji wa Simba Shaaban Kisiga (pichani) anapiga free kick tamu inayokwenda moja kwa moja wavuni huku kipa Shaaban Kado wa Coastal Union akiwa hana la kufanya. Hilo linakuwa bao la kwanza la Simba kwenye mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwana wa Taifa.
Coastal wagosi kutoka Tanga, hawakukubali, nao wakatupia wavuni bao la free kick iliyofungwa na Rama Salim kunako dakika ya 84 na kumshuhudia kipa Ivo Mapunda akiruka bila mafanikio. Likawa bao la pili la Coastal Union.
Hayo yalikuwa ni mabao yaliyopendezesha sana mchezo huo ulioisha kwa sare ya 2-2 haswa kwa namna zilivyopigwa kiufundi.
Simba iliongoza 2-0 hadi mapumziko, lakini kipindi cha pili Coast wakachomoa bao moja baada ya lingine.
Bao la pili la Simba lilifungwa na Amissi Tambwe katika dakika ya 36 akimalizia kwa kichwa kazi nzuri iliyofanywa na Emmanuel Okwi.
Coast wakachomoa bao la kwanza dakika ya 67 kupitia kwa Yayo Lutimba badaa ya gonga safi za kitabuni na wakati kipa wa Simba, Ivo Mapunda akitumia zaidi mbinu za kupoteza muda akiamini timu yake itaibuka na ushindi mwembamba, ndio ikaja free kick ya Rama Salim iliyofanya matokeo yasomeke 2-2.
Kimchezo hususan kipindi cha pili, Coast walitakata zaidi na kutandaza draft huku wakisukuma mashambulizi ya uhakika kwenye lango la Simba.
Comments
Post a Comment