BENDI ya muziki wa dansi, Kale Musica Jumamosi ilionekana kukonga vilivyo nyoyo za mashabiki waliokuwa wamefika kwa wingi kwenye ukumbi wa Kituro Night Club, Mabibo, jijini Dar es Salaam kuburudika.
Katika onesho hilo lililoanza majira ya saa 12:30 jioni, wanamuziki wa Kale wakiongozwa na Mkurugenzi Mwampashi, walionekana kuchakarika jukwaani kwa kuporomosha vibao vikali kwa mtindo wa bandika bandua.
Mara kadhaa bendi hiyo ilikuwa ikijaribu kukonga zaidi nafsi za mashabiki kwa kupiga nyimbo za miondoko mingine ya muziki kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Mwampashi, baada ya bendi yake kukubalika vilivyo kwenye onesho hilo, hivi sasa watakuwa wakitumbuiza kwenye ukumbi huo kila wiki, katika siku za Jumamosi. Wakati huohuo mcharazaji mahiri wa gitaa zito, Besi, George Gama, alivamia jukwaa la bendi ya Kale Musica na kuonyesha majabu yake katika uimbaji kwa kuimba kibao 'Nimebadilika Nini' cha Msondo Ngoma.
Tukio hilo lililotokea kwenye ukumbi wa Kituro Night Club, Mabibo, Dar es Salaam lilionekana kuwasisimua wengi, hasa kutokana na hali ya ugonjwa aliyonayo Gama ya kupooza upande wake wa kulia.
Akiwa jukwaani, Gama alionekana kuimba kwa hisia kali na kuvuta mashabiki wengi waliokuwa wakilazimika kuacha viti vyao vikiwa tupu na kujimwaga kati kucheza na wengine kumtuza.
Gama alipatwa na maradhi ya kupooza mwishoni mwa mwaka jana, ambapo amekosekana majukwaani tangu wakati huo, akijiuguza.
Comments
Post a Comment