FALSAFA NA HISTORIA YA ZAHIR ALLY ZORRO



FALSAFA NA HISTORIA YA ZAHIR ALLY ZORRO

zahir ally Zorro2  "TIJA ya kwanza na ambayo ni kubwa kabisa ya Mwalimu Nyerere kwetu sisi Watanzania ni namna alivyoweza kupinga na kuzuia matabaka kati ya
walionacho na wasionacho."

Hivyo ndivyo anavyoanza kusema mkongwe wa miondoko ya muziki wa dansi nchini, Zahir Ally 'Zorro', katika mahojiano maalum na mwandishi
wa makala hii, yaliyofanyika leo mchana.

Zorro anasema kuwa, alichokuwa akihitaji Nyerere ni kulingana ama kukaribiana kwa kipato baina ya wafanyakazi, katika kuhakikisha kila mmoja anaamini kuwa yuko sawa na mwingine.

Anasema, alichokuwa akikitaka Nyerere ni kuona kuwa hata mishahara ya wafanyakazi haipishani kiasi cha kuleta unyonge kwa wale wengine wa kima cha chini, kama ilivyo sasa.

"Hivi sasa, utakuta Meneja katika ofisi anapokea hadi shilingi milioni mbili kwa mwezi wakati mshahara wa mlinzi wake ni shilingi elfu themanini tu," anasema Zorro.

Anasema, athari mojawapo kubwa ya tofauti ya namna hiyo ya mishahara, ni hatihati ya kuendelea kuwako kwa ubepari pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.

Meneja anaweza kudiriki kumpa mlinzi elfu hamsini na kumuamuru kuiacha ofisi na kwenda kuilinda nyumba yake kwa siku moja ama hata mbili.

Zorro anasema kuwa, hali ya namna hiyo ya matumizi mabaya ya madaraka yasingekuwa rahisi kutokea iwapo mshahara wa Meneja na mlinzi ungepishana labda kwa elfu ishirini ama thelasini.

Anasema kuwa, Nyerere alikuwa kiongozi jasiri, muwazi na mpenda haki, aliyezuia wengine kujilimbikizia mali na kutumia vibaya mali za umma wakati kuna watu wanakufa njaa.

"Nafikiri, watu hawakumuelewa Nyerere ama kama walimuelewa basi walimuelewa vibaya, na matokeo yake ndio kama tunavyoona sasa, ubepari umeshika hatamu," anasema Zorro.

Akimuelezea zaidi Nyerere, Zorro anathibitisha kuwa alikuwa ni mtu mkubwa sana, ambako hatakaa atokee mwingine kama yeye hapa Tanzania.

Aidha, anaongeza kwa kusema kuwa Nyerere alikuwa binadamu wa kawaida lakini si mtu wa kawaida, kwa sababu alithubutu kukubali awe masikini kwa maslahi ya wengi.

Zaidi ya hilo, alichukua muda wake kujali maisha ya wengine ambapo aliwathamini kupita kiasi makabwela ambao hivi sasa tunawaita walalahoi, yaani watu wasio na chochote.

"Mfano wa namna alivyokuwa na utu ni jinsi alivyoondoa kodi mashuleni ili watoto wasome bure, yaani Mwalimu ni dira ya usalama wa nchi hii," anasema Zorro.

Anaeleza kuwa, namna mustakabali wa nchi unavyoendelea, inaonyesha dhahiri kuwa viongozi wa sasa wanayazingatia mafundisho ya Mwalimu Nyerere.

Zorro anaishauri serikali kuanzisha somo la 'Mwalimu Nyerere' mashuleni, ambako kupitia somo hilo, watu wamfahamu Mwalimu kuanzia darasa la kwanza.

Anasema, somo hilo la 'Mwalimu Nyerere' litamfanya kila mmoja kuijua elimu ya Mwalimu, siasa yake pamoja na ujamaa na kujitegemea kwa ujumla.

Unapomuuliza namna anavyoutazama muziki wa sasa na ule wa enzi za Mwalimu, Zorro anasema kuwa enzi za Mwalimu zilikuwa ni enzi za utu zaidi ukilinganisha na sasa.

"Enzi zile ilikuwa huwezi kuthubutu kumtaja mtu laivu kwenye nyimbo yako na kisha ukapita mitaani kutokana na misingi ya utu iliyojengeka ipasavyo wakati huo," anasema Zorro.

Zorro anasema, kwa mtazamo wake anaona kuwa muziki wa sasa umepoteza kabisa maadili na unatumika zaidi kama silaha ya kuwagombanisha watu.

Anawaasa wanajamii hususan wasanii wenzake kumuenzi Mwalimu kwa kutotumia tungo zao pamoja na vyombo vya habari kama vile magazeti kutukanana na kukashifiana.

Anasisitiza pia Watanzania kudumisha umoja, mshikamano, utulivu pamoja na amani vilivyoachwa na Mwalimu Nyerere.

"Unajua, mkifokeana watu wawili ni kama vile mbwa wanabweka, lakini mmoja tu ndio akiropoka na mwingine akikaa kimya ni vema zaidi," anasema Zorro.

Huyo ndiye Zahir Ally 'Zorro', mkongwe wa muziki ambaye ni mtunzi mahiri, mcharazaji gitaa la Solo na mwimbaji mwenye sauti inayowezakumtoa nyoka pangoni.

Alizaliwa mwaka 1954, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika shule za Kaze Hill, Kigoma na Kisarawe, Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1964 hadi 1968.

Alijipatia umaarufu mkubwa kupitia muziki hasa alipokuwa katika bendi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mafinga 'Wana Kimulimuli' aliposhiriki vilivyo kuimba pamoja na kutunga nyimbo nyingi.

Pamoja na tungo nyingi za kijamii, kadhalika, Zorro alijipatia sifa kwa kutunga na kuimba nyimbo za kuhamasisha kama vile; 'Mashujaa', 'Maneno Makini' na 'Kadi ya Chama'.

"Bendi nyingine nilizopitia na miaka yake kwenye mabano ni pamoja na Super Vea (1969) ambayo maskani yake yalikuwa ni jijini Mwanza na Mara Jazz (1973)," anasema Zorro.

Vilevile aliwahi kuzitumikia bendi kama Mwenge Jazz Paselepa (1973), Orchestra Sambulumaa (1989), Washirika Tanzania Stars (1991), Chezimba (1996) na Mas Media Group (2002).

Zorro, baba wa familia mwenye mke na watoto kadhaa wakiwamo wasanii mahiri; Banana Zorro na Maunda Zorro, anaishi jijini Dar es Salaam akijihusisha na muziki katika bendi ya B Band.



Comments