NYOTA kadhaa wa Extra Bongo wakiwemo Banza Stone, Athanas Montanabe, Adamu Bombole, Adam Hassan na wengine kadhaa, wamejiengua kwenye kundi hilo na kuanzisha bendi mpya.
Katika spidi kama ya umeme, tayari bendi hiyo mpya inayojulikana kama WANA EXTRA, imeanza kazi ambapo jana Jumapili walifanya onyesho lao la kwanza.
Wakati Chocky akiwa na Extra Bongo pale Garden Breeze Magomeni Mapipa, Banza na Wana Extra walikuwa Flamingo Bar Magomeni Mwembechai.
Akiongea kwenye jukwaa la Wana Extra, Banza Stone akasema wao ni wafungwa waliotoroka jela ya mateso.
Wakajilinganisha na ile filamu marufu ya Escape from Sobibor iliyojaa matukio ya ukatili kambini.
Banza akaiambia Saluti5 kuwa Flamingo ndio uwanja wao wa nyumbani na watakuwa wakipatikana hapo kila Jumapili.
Habari za uhakika zinadai kuanzishwa kwa Wana Extra kulianza takriban mwezi mzima ambapo mazoezi na vikao vya siri vilikuwa vikiendelea.
Inaaminika hata ndani ya Extra Bongo bado kuna virusi vya Wana Extra na haitakuwa ajabu kama wasanii wengine watachomoka kwa Ally Chocky.
Hata hivyo pamoja na kuondoka kwa wasanii hao, Extra Bongo ilitandika show safi huku Chocky akifukia vipande vingi na ilikuwa ni vigumu kubaini kuwa kuna wasanii waliomeguga.
Pichani juu kutoka kushoto ni Banza Stone, Adam Bombole na Athanas Montanabe wakiwa kwenye jukwaa la Wana Extra Jumapili usiku pale Flamingo Bar
Comments
Post a Comment