Boda Boda FC ya Karatu yanyakua kombe la virutubishi



Boda Boda FC ya Karatu yanyakua kombe la virutubishi
Wachezaji wa Boda Boda FC na washabiki wao wakishangilia ushindi baada ya kujinyakulia kombe  la virutubishi katika pambano ililofanyika katika uwanja wa Bondeni wilayani Karatu
Timu zenye upinzani wa jadi wilayani Karatu mkoani Arusha za  Boda Boda FC na Young Generation  jana zilikuwa na mpambano mkali wa mchezo  wa soka ambapo timu ya Boda Boda iliibuka na  ushindi wa mabao 2-1.

Mechi hiyo ambayo ilichezwa katika uwanja wa Bondeni chini ya udhamini wa  Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kitengo cha kutoa elimu ya virutubishi kwa jamii ilishuhudiwa na wakazi wa wilaya ya Karatu wapatao 8,000 na mgeni wa heshima alikuwa Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Karatu (OCD) Jubileth Nyange.

Timu zote 2 zilicheza kwa kujituma na kushangiliwa na wapenzi wa soka ambao ni washabiki wa timu hizo ambapo katika kipindi cha pili Boda FC ilifanikiwa kupachika mabao 2 mfululizo na wapinzani wao wakafanikiwa kurejesha bao moja.

Kwa matokeo hayo timu iliyoshinda iliweza kujipatia kombe na seti ya jezi za kisasa wakati wapinzani wao walijipatia mipira miwili kutoka kwa mdhamini.Mratibu wa  mchezo Allan Rwechungura kutoka taasisi ya Foot Print alisema lengo la  mchezo huo  lilikuwa ni kutoa burudani kwa wananchi wakati huo huo kuwapatia elimu ya lishe na matumizi ya vyakula vilivyowekewa virutubishi,kampeni ambayo inaendelea katika wilaya mbalimbali nchini chini ya usimamizi wa Wizara ya Afyana Ustawi wa Jamii.
Alisema kwa kuwa michezoni jukwaa la kukusanya watu wengi wataandaa mashindano ya michezo mbalimbali kwenye wilaya za hapa nchini ambapo timu zitakazofanya vizuri zitajipatia vifaa vya michezo wakati huo huo wananchi wataofika viwanjani kupatiwa elimu ya lishe bora na matumizi ya virutubishi lengo likiwa  ni kufikisha ujumbe wa wananchi wa kawaida.


Comments