SIMBA SC imekiri ilimsajili mshambuliaji Mkenya, Paul Raphael Kiongera akiwa majeruhi na sasa inaingia gharama za kumtibu.
Kiongera alitonesha goti lake katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili iliyopita.
Mkenya huyo aliingia kipindi cha pili, lakini dakika tano kabla ya filimbi ya mwisho akatoka baada ya kuumia, kufuatia kugongana na kipa Shaaban Kado.
Baaada ya hapo, Kiongera alikwenda kufanyiwa vipimo na kugundulika ameumia sana- hivyo atahitaji mapumziko ya wiki sita.
Hii inamaanisha uwezekano wa Kiongera kuichezea Simba SC katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ni mdogo.
Na kwa mujibu wa habari za ndani kabisa kutoka Simba SC, ni kwamba Kiongera anaweza kuwa nje ya Uwanja kwa zaidi ya muda huo.
Upo uwezekano kabisa Kiongera asiitumikie Simba SC katika mwaka wake wa kwanza kwenye mkataba wake wa miaka miwili.
Na zaidi, ataiingiza Simba SC gharama za kumtibu kwa kipindi chote hicho, huku akiendelea kulipwa stahili zake kwa mujibu wa makubaliano.
Hali kama hii iliwatokea Azam FC kwa kiungo Frank Domayo walimsajili kutoka Yanga SC akiwa majeruhi, hivyo wakaingia gharama za kumtibu na atakuwa nje hadi mapema mwakani.
Domayo naye hataitumikia Azam FC katika mwaka wake wa kwanza kwenye mkataba wake wa miaka miwili.
Ninakumbuka, mwaka 2004 Yanga SC ilimsajili mshambuliaji Patrick Kataray kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa pamoja na Pitchou Kongo.
Kongo aliitumikia vizuri tu Yanga SC kwa misimu miwili, lakini Kataray alikuwa majeruhi na hakuwahi kuutumikia vizuri mkataba wake.
Anacheza mechi mbili, mwezi mzima yuko nje anauguza nyama.
Haya yote ni matatizo ambayo yanaweza kuepukika, iwapo klabu itamfanyia vipimo mchezaji kabla ya kumsajili.
Manchester United ilikuwa tayari kumsajili Mholanzi Ruud van Nisterlooy kwa dau la rekodi katika klabu hiyo wakati huo, Pauni Milioni 18.5 mwaka 2000, lakini ikataka afanyiwe vipimo vya kina kutokana na hofu ya maumivu yake ya goti.
Lakini United iliamua kuachana na mchezaji huyo, baada ya klabu yake wakati huo, PSV Eindhovein kukataa mshambuliaji huyo kufanyiwa vipimo vya kina na siku moja baada ya kukataa, Van Nisterlooy akaumia goti lililomuweka nje kwa mwaka mzima.
Lakini mwaka mmoja, baadaye United ilimnunua mchezaji huyo kwa Pauni Milioni 19 na akaichezea timu hiyo hadi mwaka 2006 alipotimkia Real Madrid.
Vipimo vya afya ni jambo muhimu- hata kama klabu imempenda mchezaji na kuamua kumsajili akiwa na maumivu, lakini aina ya Mkataba itakuwa tofauti.
Watu wananunua magari yenye dosari, lakini kwa utashi wao na kwa bei ambazo zinaendana na magari yenyewe, wakijua kabisa wataingia gharama za marekebisho.
Wazi Simba SC ilimsajili Kiongera kama mchezaji fiti na anayeingia moja kwa moja kufanya kazi- hivyo hata Mkataba wake ulizingatia hayo.
Lakini kama mchezaji huyo angepimwa afya vizuri na tatizo likajulikana, naamini Mkataba wake ungekuwa tofauti na ule ambao upo kwenye makabati ya Simba SC hivi sasa.
Vile vile kwa Azam na Domayo, kama angefanyiwa vipimo kabla ya kusajiliwa, Mkataba wake ungezingatia hali yake- lakini kwa kuwa watu wanaingia 'kichwa kichwa' matokeo ndiyo haya.
Comments
Post a Comment