SHIKAMOO Jazz Band 'Wana Chelachela Beat', ni kundi la muiziki          wa dansi lilianzishwa mwaka 1993 kwa kujumuisha baadhi ya nguli          wa miondoko hiyo kutoka katika bendi nyingine kadhaa.
          Nguli hao ni Salum Zahor, John Simon, Ally Adinani, Athuman          Manicho, Ally Rashid, Kassim Mapili na wengine ambao ni          marehemu, akina Mohammed Tungwa, Kassim Mponda na Mariam Nylon.
          Mbali ya hao, kuna mwanamuziki mwingine nguli katika upulizaji          wa Domo la Bata 'Saxophone', aliyepitia bendi kadha wa kadha za          muziki wa dansi, Bakari Majengo.
          Akiwa mmoja wa waasisi wa Shikamoo Jazz, Majengo amechangia          mafanikio makubwa ndani ya bendi hiyo, ikiwa ni pamoja na          kuiongezea mashabiki na kuvuta mapromota nje ya nchi.
          Majengo anamtaja mzungu aitwaye Ronnie Graham aliyekuwa          anafanyakazi katika shirika la Help Age Tanzania, kuwa ndiye          chanzo cha Shikamoo Jazz.
          Ronnie akiwa HelpAge alikuwa na kamati iliyokuwa na wajumbe kama          John Kitime, Mariam Hamdani, marehemu Godigodi ambayo ndiyo          iliyowezesha ujaji wa vyombo vya muziki kutoka Uingereza na          baada ya hapo Godigodi na Kitime ndio walienda nyumbani kwa Mzee          Salum Zahoro na kumtaka akusanye wakongwe wenzie watengeneze          kundi lililokuwa chini ya Helpage na kuwa ni njia moja wapo ya          shirika hilo kuwezesha wazee kujitegemea.
          Anasema kuwa, tangu ajiunge na bendi hiyo ambayo awali maskani          yake yalikuwa Tanzania Region, ameshasafiri nayo nchi kadhaa,          zikiwamo Kenya na Uingereza.
          Ronnie aliamua kuiacha bendi hiyo kutokana na vituko          vilivyofanywa na mmoja wa wazee hao bendi ilipoenda Uingereza.
          Kutokana na waanzilishi wengine kuwa wameshafariki, ni          wanamuziki wanne tu wanaoiendesha Shikamoo Jazz Band sasa, ambao          ni Salum Zahor, John Simon, Ally Adinani na yeye mwenyewe.
          Akizungumzia historia yake kimuziki, Majengo anasema kuwa, mwaka          1954 ndipo alipoanza kujiingiza kwenye fani hiyo kwa kujiunga na          bendi ya Dar es Salaam Jazz, akiwa mkung'utaji Tumba.
          Kabla ya hapo, Majengo anasema kuwa, alikuwa akipiga ngoma          kwenye vibendi vya watoto na kutumbuiza katika sherehe          mbalimbali za kichama, kwenye ofisi za TANU.
          Baadhi ya wanamuziki waliompokea Dar es Salaam Jazz, ni pamoja          na Edward Salvu na Grey Sindo waliokuwa mahiri kwa upulizaji          Sax, ambao kwa nyakati tofauti walichangia kumnoa kwenye chombo          hicho.
          Ilipofika mwaka 1963, marehemu King Michael Enock aliingia Dar          Jazz na kumuongezea ujuzi wa kupuliza Sax kwa kiwango kikubwa.
          Mwaka 1968 aliondoka Dar Jazz akiwa keshashiriki kupiga Sax          kwenye vibao vingi, kikiwamo kile maarufu, 'Mtoto Acha Kupiga          Mayowe', akajiunga na bendi ya Wakongoman watupu iliyoitwa King          Afrika.
          Mwaka 1969 alijiunga na bendi nyingine ambayo nayo ilikuwa ya          Wakongoman, iliyoitwa 60 Zaire, kabla ya mwaka 1970 kuingia Nova          Success ya Papaa Micky, saksafoni katika nyimbo kama Chlorida na          kadhalika ni kazi ya Majengo.
          Aliachana na Nova Success mwaka 1974, bendi ilipopata safari ya          Swaziland ambapo yeye alishindwa kwenda kutokana na ajira          aliyokuwa nayo katika kiwanda cha BATA Shoes, jijini Dar es          Salaam.
          Alifanyakazi kazi kwenye kiwanda cha BATA tangu mwaka 1963.          Mwaka 1975 aliingia Maquis Original 'Wana Kamanyola' iliyokuwa          chini ya mpulizaji Sax hodari, Chinyama Chiaza, akashiriki          kurekodi vibao vingi zaidi vya bendi hiyo, huku mwenyewe akisifu          kazi aliyoifanya katika wimbo 'Nimepigwa Ngwala'.
          Akiwa Maquis, mwaka 1986 alisimama kufanyakazi kutokana na          kusumbuliwa na maumivu ya kifua na alipopata nafuu, alikwenda          kumsaidia mwanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango 'King Kikii'          aliyekuwa kaanzisha bendi yake ya Orchestra Double O.
          Chinyama alipobaini hilo, alimfuata na kumuomba arudi Maquis,          ambapo siku aliyorejea kazini alikuta bendi iko chini ya          Tshimanga Kalala Assosa ambaye wakati huo walikuwa hawajuani.
          "Nilisalimiana naye kikawaida lakini nilipotaka kupanda jukwaani          alinizuia akitaka nimsujudie kumuomba kwa vile yeye ndie          Kiongozi, baada ya majibizano nilisusa na kusimama bendi,"          anasema Majengo.
          Majengo anasema kuwa, alipokuwa kasimama kuitumikia Maquis, siku          moja alitembelea onesho la pamoja na OSS 'Wana Power Iranda' na          mmiliki wa OSS, Huggo Kisima alipomuona akamvuta kwake, na          Septemba 1986 alianza kazi rasmi na wanamuziki Muhidin Gurumo,          Skassy Kasambulla na Abdallah Kimeza ndani ya OSS na kushiriki          kurekodi nao vibao vingi vikiwamo 'POP' na 'Mbu'.
          Mwaka 1990 alirudi tena Maquis na kushiriki nao hadi mwaka 1993          alipoachia ngazi rasmi na kuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo          Jazz.
          Tofauti na wanamuziki wengi wanaotupa lawama kwa vyombo vya          habari kuhusiana na kudidimia kwa dansi, Majengo anaweka wazi          kuwa, ubinafsi wa wanamuziki wenyewe ndio chanzo.
          Majengo anasema kuwa, kila mmoja kwenye muziki wa dansi          anajijali yeye mwenyewe na wanamuziki wake tu na kwamba          ushirikiano uliopo ni wa mdomoni si wa vitendo.
          Faida aliyoyapata Majengo katika kazi ya muziki anayoielezea          kuwa ni ngumu kufanikiwa kwa sasa, ni kufanikiwa kujenga nyumba          maeneo ya Kigogo Luhanga, jijini Dar es Salaam.
          Kwa upande wa familia, Majengo anayefurahia watoto wake          kutorithi kazi yake ya muziki, ana mke na watoto watano, ambao          ni Selemani, Kassim, Juma, Zubeda na Tunu.
          Alizaliwa mwaka 1943, Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kupata          elimu ya msingi katika shule ya Mchikichini kwa miaka miwili ya          1949 na 50.
          Mwaka 1955 ilipoanzishwa shule ya Magomeni Mzimuni, alilazimika          kuanza tena darasa la kwanza hadi la nane mwaka 1962.
Comments
Post a Comment