TUMPE HESHIMA YAKE CHRISTIAN BELLA …Dar es Salaam yatingishika, Usiku wa Nani Kama waielemea Mzalendo Pub
UKUMBI kujaa kupitiliza - kuliko wakati wowote ule huko nyuma, kuwaimbisha mashabiki vile alivyotaka, kwenda na muda, kushambulia jukwaa vile inavyostahili, mashabiki kutohofia mvua, ni sehemu tu ya vitu vilivyothibitisha kuwa Christian Bella yuko katika sayari ya peke yake kwenye muziki dansi hapa bongo.
Hiyo ilikuwa ni Ijumaa usiku kuamkia Jumamosi hii, ambayo Christian Bella aliyesindikizwa na bendi yake ya Malaika, alifanya tukio kubwa la burudani kwa kushuka na onyesho lake la Nani "Kama Kama Mama" lililofanyika ndani ya ukumbi wa Mzalendo Pub Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Mzalendo Pub ilielemewa, onyesho halikuwa saizi yake - umati uliofurika pale utaendelea kubaki kama historia isiyofutika mbele ya mashuhuda wa onyesho hilo.
Katika onyesho hilo Bella akaweza kufanya show iliyowashirikisha pia nyota wa muziki wa kizazi kipya kama vile Ommy Dimpoz, Banana Zorro, Matonya na Cassim Mganga lakini bado hakuna aliyeweza kumfunika – jamii ikashuhudia mwimbaji wa muziki wa dansi akichanua mbele ya waimbaji wa bongo fleva na kujipambanua kwa uwazi kabisa kuwa ni msanii aliyeenea kila idara.
Ni wazi kuwa ni mchawi tu ndiye anayeweza kuukataa ukweli kuwa Bella ndiye balozi wa muziki wa dansi.
Wimbo Nani Kama Mama uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu, ukaufanya ukumbi wa Mzalendo Pub uzizime. Hata manyunyu ya mvua yaliyokuwa yakidondoka katika muda mwingi wa onyesho hilo, hayakuwa tatizo.
Wasanii wa bendi ya Malaika waliokuwa jukwaani kuhakikisha nyimbo zote zinakwenda live – kuanzia zile za kwao hadi za bongo fleva, walikuwa smati na kufanya jukwaa liwe na mvuto wa aina yake. Kama bendi hii itamudu kuhimili mawimbi angalau kwa mwaka mmoja mbele, basi Tanzania itakuwa imebahatika kuwa na bendi yenye wasifu wa kipekee yenye mapigo ya kipekee, nyimbo za kipekee na wasanii wa kipekee.
Comments
Post a Comment