TUKUBALI TUSIKUBALI CHRISTIAN BELLA NDIYE BALOZI WA MUZIKI WA DANSI …makubwa yasubiriwa katika Usiku wa Nani Kama Mama Ijumaa hii
HII inaweza kuwa ngumu kumeza kwa baadhi ya wanamuziki wa dansi, lakini ndio ukweli wa mambo – Christian Bella ndiye mwanamuziki pekee wa dansi anayewakilisha kwenye majukwaa ya matamasha makubwa ya Fiesta na Kili Tour yanayoendelea sehemu mbali mbali hapa nchini.
Hadi sasa hivi hakuna mwanamuziki wa dansi aliyenusa kwenye matamasha hayo, ni Bella pekee anayechanja mbuga kwa kushiriki maonyesho mengi ya Fiesta na Kili Tour.
Jamaa anatengeneza mtonyo ile mbaya – sio siri kuwa kwa sasa yeye ndiye mwanamuziki wa dansi anayeingiza pesa nyingi kutokana na maonyesho binafsi achilia mbali kipato anachoingiza kupitia bendi yake ya Malaika.
Alipoulizwa na Saluti5 anajisikiaje kuwa mwanamuziki pekee wa dansi anayetesa kwenye matamasha ya Fiesta na Kili, Bella hakutaka kutamba wala kujikweza – akasema kama wapo wanaostahili kujisikia vyovyote vile kwa hali hiyo basi ni mashabiki wake ambao ndio wamemfikisha hapo alipo.
Bella akaongeza kuwa kwasasa angependa kuzungumzia kitu kimoja – Usiku wa Nani Kama Mama utakaofanyika Ijumaa hii katika ukumbi wa Mzalendo Pub pale Millennium Pub Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
"Hii ni show yangu maalum, nimekusudia kufanya mambo makubwa, wimbo wa Nani Kama Mama umekuwa mkubwa sana, umeniongezea mashabiki wengi, sijawahi kuupiga live popote pale, hilo litatokea Ijumaa Mzalendo Pub," alisema Bella.
"Nini nimekifanya kwenye Fiesta na Kili Tour kitaonekana punde kwenye TV mbali mbali pamoja na mitandaoni, sina haja ya kuandikia mate ila kwa sasa akili yangu yote nimeilekeza kwenye Usiku wa Nani Kama Mama," aliongeza Bella.
Katika usiku wa Nani Kama Mama, Bella anategemewa kuzindua albam aliyoitambulisha kama Volume 1 ambayo itakuwa na nyimbo 6. Itapatikana katika Audio CD na DVD.
Moja ya siri ya mafanikio ya Bella ni kuweza kuibuka na tungo pamoja na nyimbo ambazo zimemudu kuchuana vikali na nyimbo za bongo fleva ambazo hakuna shaka kuwa kwa sasa zimetibua soko la muziki wa dansi.
Je Bella anaahidi nini juu ya show ya Usiku wa Nani Kama Mama? ingia Saluti5 kesho, utamskia live.
Comments
Post a Comment