WINGA wa Real Madrid Angel Di Maria anazidi 'kunukia' Manchester United baada ya kocha wake Carlo Ancelotti kufichua kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina ameaga rasmi wachezaji wenzake.
Di Maria yuko kwenye harakati za kwenda Old Trafford ikionekana wazi kuwa atakuwa mchezaji aliyenunuliwa kwa bei mbaya kuliko yeyote yule katika Premier League ambapo Manchster United wanatarajiwa kulipa zaidi ya pauni milioni 60 kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 24.
Manchester United walitarajia kulipa pauni milioni 56 kwa Di Maria, hata hivyo inasemekana Real Madrid wamepandisha bei katika kipindi hiki ambacho wanajua wazi kuwa kocha wa United Van Gaal anamtaka mshambuliaji huyo kwa udi na uvumba.
Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari, Ancelotti alisema yafuatayo juu ya winga huyo wa zamani wa Benfica: " Di Maria ametuaga. Tunamshukuru kwa kila jambo alilofanya kwa klabu.
"Tumejaribu kwa kila hali kumzuia lakini ameamua kwenda sehemu nyingine. Tunamtakia kila la kheri".
Di Maria ambaye anatarajiwa kuvaa jezi namba 7 Old Trafford, anategemewa kupokea mshahara wa pauni 200,000 kwa wiki.
Comments
Post a Comment