KAMA Liverpool wanadhani wana ubavu wa kupimana nguvu na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City basi wakajipange upya.
Liverpool inayojinasibu kusaka ubingwa wa Ligi Kuu, imejikuta ikiambulia kipigo cha 3-1 kutoka kwa Manchester City kwenye uwanja wa Etihad Jumatatu usiku.
Ikishuhudiwa na mchezaji wao mpya Mario Balotteli aliyekuwa jukwaani kufuatilia mchezo huo, Liverpool ikakukuruka hadi dakika ya 41 kabla ya kuruhusu bao la kwanza lilifungwa na Stevan Jovetic aliyekuwa nyota wa mchezo.
Dakika ya 55, kwa mara nyingine tena Jovetic akawafanya Liverpool waende nyavuni kuokota mpira baada ya kufunga tamu lililotokana na pasi 19.
Zilikuwa ni gonga za aina yake ambapo ukingoni mwa gonga hizo Stevan Jovetic alimpa pande Samir Nasir na kukimbia mbele kusubiri arudishiwe mpira na Nasiri na ndivyo ilivyokuwa – akarudishiwa mpira na kumtungua kipa Mignolet, mashabiki wa City wakaingia wazimu.
Sergio Aguero aliyeingia dakika ya 69 kuchukua nafasi za Dzeko akaipatia City bao tatu sekunde chache tu baada ya kuingia uwanjani.
Liverpool, timu ya pili duniani kwa kumwaga pesa nyingi kwenye usajili msimu huu, ikasubiri hadi dakika ya 83 kupata goli la zawadi kutoka kwa beki wa City, Zabaleta aliyejifunga mwenyewe.
Comments
Post a Comment