HUYU NDIYE HUSSEIN KIHATE MWALIMU WA MUZIKI WA MUUMIN NA ALLY CHOCKY …aliwatoa pia Nasir Lubua, Badi Bakule na Jado FFU
WAKO watu wengi waliotia mkono wao katika kuwanoa wanamuziki nyota Mwinjuma Muumin na Ally Chocky lakini mzee Hussein Kihate anahitaji heshima ya kipekee katika hili.
Huyu ndiye mwalimu aliyewapika kimuziki Muumin na Chocky kabla hawajaingia kwenye mikono ya watu wengine.
Hussein Kihate alikuwa mmliki wa bendi ya Lola Afrika iliyodumu kati ya kipindi cha mwaka 1975 na 1990 ambapo kupitia bendi hiyo aliwatengeneza wanamuziki kadhaa wakiwemo Chocky, Muumin, Badi Bakule, Munsemba wa Minyigu na Jado FFU.
Katika orodha ndefu ya wasanii waliopita kwenye mikono ya Hussein Kihate wapo pia marehemu Nasir (Francis) Lubua aliyetamba na Sikinde, marehemu Mbwana Cocks aliyetesa na Maquis pamoja na marehemu Aggrey Ndumbalo.
Kihate ameiambia Saluti5 kuwa bendi yake ilikufa kifo cha kawaida kutokana na uchakavu wa vyombo pamoja na kuchukuliwa mara kwa mara kwa wasanii wake.
Hussein Kihate ambaye alikuwa mwimbaji, mcharaza gitaa la solo na mtunzi, anawataja Muumin, Chocky na Jado kama wanafunzi wake 'wapiganaji' ambao anaamini wameutendea haki ujuzi waliouchota kwake.
"Hawa ni vijana wahangaikaji na wapiganaji, wamepigania maisha yao kupitia muziki hadi nje ya mipaka ya nchi – walikaa Kenya kwa muda mrefu na kufanya vizuri," alisema Kihate ambaye kwasasa hajishughulishi tena na muziki.
Muumin aliiambia Saluti5 kuwa ni kwa Hussein Kihate ndipo alipoanza a-e-i-o-u kwenye muziki.
"Dancan Ndumbalo alinichukua mimi na mdogo wake (Aggrey Ndumbalo) na kutupeleka kwa Kihate kwaajili ya kufundishwa muziki. Pale Lola Afrika ndio ilikuwa kama shule yetu," alisema Muumin
Pichani juu ni Muumin akiwa na mzee Hussein Kihate.
Comments
Post a Comment