HAYAWI HAYAWI SASA YAMEKUA …TWANGA PEPETA NA FM ACADEMIA KUPAMBANA JUKWAA MOJA …watazunguka mikoa saba
MECHI iliyotafutwa kwa miaka mingi bila mafanikio, hatimaye sasa imekubalika – African Stars "Twanga Pepeta" na FM Academia "Wazee wa Ngwasuma" wataumana jukwaa moja baadae mwaka huu.
Saluti5 imepenyezewa habari za ndani kabisa kuwa baada ya majadiliano mazito, bendi hizo mbili zimekubalina kwa PAMOJA kuandaa kwa PAMOJA onyesho la PAMOJA – hakuna promota - watagharamia kwa pamoja tukio hilo na kuvuna kwa pamoja kile watakachojaaliwa kukichuma.
Onyesho litafanyika kati ya mwezi Oktoba au Novemba jijini Dar es Salaam katika ukumbi utakaotajwa baadae na baada ya hapo watakwenda kulirudia onyesho hilo katika mikoa saba.
Saluti5 imeambiwa kuwa hata ma-mc wa onyesho hilo la Dar es Salaam wameshapendekezwa – mmoja akitarajiwa kutoka Clouds na mwingine TBC.
Hapo awali juhudi za kuzikutanisha FM Academia na Twanga Pepeta zilikuwa zikigonga mwamba ambapo kila wakati bendi moja iliyojiona iko juu zaidi kibiashara ilikuwa ikichomoa kufanya onyesho la pamoja – mara FM wachomoe, mara Twanga wachomoe.
Bendi hizi pinzani zimewahi kukutana kiaina kwenye maonyesho machache ya kutumbuiza nyimbo moja moja ikiwemo show za Miss Tanzania na Fiesta.
Lakini hili sasa litakuwa onyesho la kwanza rasmi litakalowapambanisha jukwaani mahasimu hao ambao wametawala soko la muziki wa dansi kwa muda mrefu.
Onyesho hili la aina yake na la kihistoria bila shaka litachochea kuunyanyua upya muziki wa dansi ambao kwa miaka ya hivi karibuni umekuwa ukididimia. Ni wazo linalostahili pongezi za hali ya juu.
Comments
Post a Comment