VAN GAAL AANZA KWA KISHINDO MAN UNITED IKIICHAPA LA GALAXY 7-0 …Rooney atupia 2, Fletcher nahodha, Herrera atakata ile mbaya
KOCHA Louis van Gaal ameanza vizuri kibarua chake Manchester United baada ya kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa bao 7-0 dhidi ya LA Galaxy katika mchezo wa kirafiki uliochezwa nchini Marekani.
Mshambuliaji Wayne Rooney ameanza vizuri kampeni yake ya kumshawishi Van Gaal juu ya uwezo wake uwanjani baada ya kutupia wavuni mabao mawili.
Roonye alifunga katika dakika ya 42 na 45 wakati huo tayari United ilikuwa mbele kwa bao moja lililofungwa na Welbeck dakika ya 13.
Mchezaji kutoka kikosi cha vijana Reece James mwenye umri wa miaka 20, akicheza mechi yake ya kwanza kwa timu ya wakubwa naye akafunga mara mbili katika dakika ya 62 na 84.
Winga Ashley Young aliyeingia kipindi cha pili naye pia akatupia mipira wavuni mara mbili dakika ya 88 na 90.
Kiungo mpya wa United, Herrera alitakata sana katikati ya dimba na kutengeneza mabao mengi ambapo yeye na kiungo mwenzake Darren Fletcher ndio wachezaji pekee waliocheza kwa dakika 90 huku karibu ya nusu ya timu ikibadilishwa kipindi cha pili.
Fletcher ndiye aliyekuwa nahodha wa mchezo huo.
Kikosi cha United kilichoanza kilikuwa hiki:De Gea, Smalling, Jones, Evans, Valencia, Fletcher, Herrera, Shaw, Mata, Welbeck, Rooney.
Kikikosi kilichoingia kipindi cha pili ni: Lindegaard; Rafael, M Keane, Fletcher, Blackett, James; Kagawa, Cleverley, Herrera; Nani, Young.
Comments
Post a Comment