TOM OLABA ASAKA `STEPU` YA KUCHEZA MUZIKI WA LIGI KUU MSIMU UJAO!

 
Kocha mkuu wa Ruvu Shooting, Mkenya Tom Alex Olaba amewaamini vijana wake chini ya umri miaka 20
KOCHA mkuu wa Ruvu Shooting, Mkenya Tom Alex Olaba amedhamiria kukijenga upya kikosi chake kwa kuwapa uzoefu vijana wenye umri chini ya miaka ishirini (U-20) waliowapandisha kutoka timu B na wale waliosajiliwa wakati wa majaribio.Ruvu Shooting aliwafanyia majaribio wachezaji vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania mwezi mei mwaka huu na wale waliofuzu walijiunga na timu B.Ikiwa ni sehemu ya kuwaimarisha na kuwapa uzoefu wa kucheza ligi kuu, Olaba anawapa nafasi ya kucheza mechi mbalimbali za kirafiki.
Kocha huyo aliyefungwa bao 1-0 na Azam jana katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es salaam alisema vijana wake hawajapata uzoefu, lakini wanaonekana kucheza vizuri na kadiri siku zinavyokwenda hofu inawatoka.
"Ukiangalia jinsi tulivyocheza mechi ya kirafiki na Azam fc, utagundua haraka haraka kuwa vijana wa U-20 walikuwa na wasiwasi,". Alisema Olaba.
Msimi uliopita, Ruvu Shooting walifungwa mabao 7-0 dhidi ya Yanga sc uwanja wa Taifa

"Kipindi cha kwanza tulicheza vizuri sana, lakini kipindi cha pili wao wakapata goli moja. Kufungwa kwangu,  mimi sina neno. Nina maana yangu ya kucheza ya mechi za kirafiki".
"Niliwaweka U-20, ndio mara yao ya kwanza kucheza na Azam, ukiwatazama unaona walitetemeka. Azam wengi wao ni wachezaji wa kigeni, wachezaji wangu wa U-20 wamepata uzoefu mkubwa. Aliongeza Olaba.
Aidha, Olaba alisema kuwa anatarajia kucheza mechi nyingi zaidi za kujipima uwezo baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, lengo likiwa ni kukisuka kikosi kwa ajili ya ligi kuu inayotarajia kuanza kushika kasi septemba 20 mwaka huu..
"Nitacheza mechi nyingi sana, hata hivi leo  ninacheza na JKT Ruvu Stars hapa kwetu Mabatini. Baada ya sikuu ya ramadhani nitacheza mechi nyingi sana, siwezi kutaja idadi". Aliongeza Olaba.
"Kila kocha anapocheza mechi za kirafiki anaona makosa, akirudi nyumbani anaenda kurekebisha".
Msimu uliopita, Olaba aliyerithi mikoba ya aliyekuwa kocha mkuu na akatimkia Yanga sc, Charles Boniface Mkwasa `Master`  aliiongoza Ruvu Shooting kushika nafasi ya 6 katika msimamo wa ligi kuu kwa kujikusanyia pointi 38 kibindoni.

Walishinda mechi 10, walitoka sare mechi 8 na kufungwa mechi 8. Idadi ya mabao waliyofunga yalikuwa 28 na walifungwa mabao 32.

Comments