TAMBO ZA MTIBWA SUGAR TIMU PINZANI ZINAWEZA KUKIMBIA LIGI KUU



TAMBO ZA MTIBWA SUGAR TIMU PINZANI ZINAWEZA KUKIMBIA LIGI KUU
 Kikosi cha Mtibwa Sugar msimu uliopita. Mlinda mlango Hussein Sharrif `Casillas` amejiunga na Simba majira haya ya kiangazi na kusaini mkataba wa miaka miwiliTIMU nyingi zinazoshiriki ligi kuu soka Tanzania bara zipo katika maandalizi ya kujiwinda na msimu mpya utakaoanza kushika kasi septemba 20 mwaka huu.Wakata miwa wa mashamba wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar wapo jijini Dar es salaam kujifua katika fukwe za Koko ili kujiimarisha zaidi.
Mtibwa Sugar chini ya kocha mkuu, Mtanzania Mecky Mexime, msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya 7 kwa kujikusanyia pointi 31 kibindoni.
Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Tanzania kwa mwaka 1999 na 2000 walishinda mechi 7, sare 10 na kufungwa mechi 9. Walitikisa nyavu za wapinzani mara 30 na zao kuguswa mara 31.
Tangu itwae ubingwa miaka miwili mfululizo (1999, 2000), Mtibwa haijawahi kuwa katika ubora wake na kujikuta ikishika nafasi za kawaida katika msimamo.
Msimu uliopita walishindwa kutamba kabisa na kuziacha timu za Azam fc, Yanga, Mbeya City fc, Simba, Kagera Sugar na Ruvu Shooting kukaa juu yao katika msimamo wa ligi kuu.
Mtibwa ni timu inayoendeshwa kikampuni na haina matatizo kama klabu za wanachama, lakini haijawa na makali kama Azam fc na hata pacha wao  Kagera Sugar.
Kuelekea msimu ujao, wakata miwa hao wa Manungu wamesema wanajifua vilivyo ili kurejesha heshima yao iliyopotea kwa muda mrefu.
Afisa habari wa klabu hiyo, Tobias Kifaru Lugalambwika amejitapa na kusema kwamba maandalizi yanakwenda vizuri na wala hakuna haja ya kuifananisha na timu ndogo.
"Mtibwa iko vizuri kweli kweli, moja ya klabu inayoendeshwa kikampuni, Tunakwenda kwenye mstari, hatuyumbishwi na watu". Alisema Kifaru.
Afisa habari huyo aliongeza kuwa Mtibwa ni klabu bora Tanzania, tofauti na timu changa za Azam na Mbeya City.
" Hapa Tanzania klabu bora na kongwe ni tatu tu, Simba, Yanga na Mtibwa". Alijigamba Kifaru.
"Kuna timu zinawika mwaka mmoja halafu zinatelemka, halafu unaziona tena baada ya miaka 10 au 15. Mtibwa ipo juu na usifananishe ni timu nyingine".

"Maandalizi ni mazuri na msimu ujao tutafanya vizuri na kurudi katika hadhi yetu. Tunakiri kufanya vibaya kwa miaka mingi, lakini sasa inatosha". Alimaliza Kifaru.


Comments