Straika wa England atua Yanga, aanza mazoezi


YANGA kweli ngoma inogile! Ndivyo unaweza kusema, baada ya mshambuliaji mwingine kutua klabuni hapo akitokea England na kisha kuanza mazoezi chini ya Kocha Marcio Maximo.
Mshambuliaji mpya wa Yanga aliyekuwa akikipiga katika timu ya Coventry City ya England Suleiman Abdallah Mbarouk.
Mshambuliaji huyo raia wa Tanzania ambaye amekuwa akicheza soka England kwa miaka mingi, Suleiman Abdallah Mbarouk, aliyekuwa akikipiga katika timu ya Coventry City ya England inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, alijumuika mazoezini kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola jijini lakini bado hajapewa mkataba wowote.

Taarifa kutoka klabuni hapo zinaeleza kuwa, Maximo amekabidhiwa mchezaji huyo kwa ajili ya kumfanyia majaribio na kama akionekana anaweza, atapewa mkataba.
Championi Ijumaa, lilizungumza na mchezaji huyo ambapo alisema amerejea nchini kwa kuwa mkataba wake na klabu yake nchini England ulimalizika na hakuwa kwenye mipango ya timu yoyote.
Suleiman Abdallah Mbarouk akiwa na Jaja.
"Nimeachana na Coventry City mwaka mmoja hivi uliopita, niliumia mgongo, hivyo nikawa nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita, lakini hivi sasa nimepona, nahitaji kuendeleza kipaji changu cha soka.
"Wakala wangu, anaitwa Salim ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Afri-Soccer cha Zanzibar, ndiye amenileta hapa kwa ajili ya majaribio, nilianzia Simba na sasa nimekuja kujaribu Yanga."
Mchezaji huyo ambaye alisema kabla ya kutua Coventry City aliwahi kupata mafunzo ya soka katika kituo cha Chelsea cha England, hakuonyesha uwezo mkubwa katika mazoezi ya jana, hata Maximo pia hakutaka kuzungumza chochote juu yake.
Gazeti hili lilipotafuta takwimu na rekodi zake lilibaini kuwa aliwahi kuichezea timu ya watoto ya  Coventry City, lakini kama anahitaji kupata nafasi kweli kwenye kikosi cha Yanga, basi kazi kubwa ipo mbele yake.

Comments