SIMBA SC YAMNASA ELIAS MAGURI KUTOKA RUVU SHOOTING



SIMBA SC YAMNASA ELIAS MAGURI KUTOKA RUVU SHOOTING
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KLABU ya Simba sc imemalizana na klabu ya Ruvu Shooting kuhusu kumsajili mshambuliaji wa maafande hao, Elias Maguri .
Afisa habari wa klabu hiyo, Masau Bwire amesema wakati wa sikuu ya Eid El Fitri, Simba walipeleka ofa, wakakaa pamoja na kujadili na hatimaye kufikia makubaliano.
"Simba wamefuata taratibu zote, wamekuja kwetu,  kwasababu Maguri ana mkataba na sisi. Tumekubaliana na kilichobaki ni mchezaji mwenyewe kumalizana na Simba kwa maslahi binafsi," alisema Masau.
Masau aliongeza kuwa kwasasa Maguri yupo kambini Ruvu Shooting na anasubiriwa na Simba ili wakafikie makubaliano binafsi ili asaini mkataba.
Maguri ni miongoni mwa washambuliaji waliokuwepo katika mipango ya kocha mkuu wa Simba, Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Awali Ruvu Shooting waliwashutumu Simba kutaka kufanya usajili wa kinyemela na kuwataka wafuate taratibu zote zinazotakiwa kwasababu wao wana haki zote za mchezaji.
Simba walifyata mkia na kuwafuata Shooting ambapo sasa wamefikia makubaliano baina ya pande zote mbili. Hata hivyo ada ya uhamisho ya Maguri haijawekwa wazi.



Comments