MAGWIJI wa muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma Music Band 'Mambo Hadharani' na Mlimani Park Orchestra "Sikinde Ngoma Ya Ukae" leo mchana watachuana vikali katika viwanja vya TCC Club Chang'ombe, Temeke.
Mpambano huo wa Nani Mtani Jembe ni kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitri na pia litaamua ni bendi ipi kali kati yao.
Mratibu wa mchuano huo, Joseph Kapinga amesema pambano hilo litaanza saa nane alasiri hadi majogoo.
Kapinga alisema bendi zote mbili ziliwasili jana kutoka msituni walipojificha kujiandaa na mpambano huo.
Mratibu huyo alisema kila bendi itapiga kwenye jukwaa lake ili kulinda upinzani wao.
Katika pambano hilo, Msondo ndiyo watakaoanza kupanda jukwaani na baadaye Sikinde watakuwa wakijibu mashambulizi.
Kiongozi wa Msondo Ngoma Saidi Mabera alisema jana watapiga nyimbo zao zote kali ili kuhakikisha wanaisambaratisha Sikinde.
Baadhi ya wanamuziki wanaounda Msondo Ngoma ni Shaaban Dede, Mabera, Eddo Sanga, Juma Katundu, Roman Mng'ande `Romario' na Hassan Moshi.
Naye kiongozi wa Sikinde Hamisi Mirambo alijigamba kuwa wataibuka na ushindi mnono.
"Tuna waimbaji wazuri na hakuna itakachotuzuia kushinda," alisema Mirambo.
Baadhi ya wanamuziki wanaounda Sikinde ni Hassan Rehani Bitchuka, Hassan Kunyata, Abdala Hemba, Musemba Waminyugu.
Ramadhani Mapesa, Adofth Mbinga, Kelvin Mausi Mjusi Shemboza, Tonny Karama, Bonny Bass, Habibu Abass Jeff , Juma, Juma Choka, Mbaraka Othman, Hamisi Mirambo, Ali Yahaya, Yusuph Benard na Ali Jamwaka.
Pambano imeandaliwa na Keen Arts na Bob Entertainment chini ya udhamini wa Konyagi na Saluti5.
Comments
Post a Comment