Mkurugenzi Sera na                Utafiti wa TRA Bw. Tonedeus Muganyizi akizungumza na wana                umoja wa uingizaji na uuzaji wa kazi za filamu na muziki                zinazotoka nchi za nje wakati wa kikao cha wafanyabiashara                hao na asasi zinazosimamia usambazaji na uuzaji wa kazi za                filamu na muziki jana jijini Dar es Salaam. 
                Wadau mbalimbali                wakijadiliana wakati wa kikao cha wafanyabiashara na asasi                zinazosimamia usambazaji na uuzaji wa kazi za filamu na                muziki jana jijini Dar es Salaam. 
        Na Genofeva Matemu –                Afisa Mawasiliano Serikalini WHVUM 
         Mkurugenzi Sera na                Utafiti kutoka TRA Bw. Tonedeus Muganyizi amevitaka vyombo                vya udhibiti vya kiserikali kufanya kazi kwa pamoja na TRA                katika kusimamia sheria na kanuni za usambazaji na uuzaji                wa kazi za Filamu na muziki nchini.
        Rai hiyo jana jijini Dar                es Salaam wakati wa kikao kilichowahusisha wafanyabiashara                wanaosambaza kazi za filamu na muziki pamoja na wadau                wanaohusika na usimamizi wa usambazaji wa kazi za filamu                na muziki kutoka TRA, Bodi ya Filamu, BASATA, pamoja na                COSOTA baada ya wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi yao                kuhusiana na operesheni inayoendelea ya kukamata kazi za                filamu na muziki zinazotoka nje ya nchi zisizokuwa na haki                miliki na stempu ya TRA.
        Aidha Bw. Muganyizi                amesema kuwa kazi yoyote ya filamu na muziki inapaswa kuwa                na haki miliki kabla ya kusambazwa ili kuiwezesha TRA                kutoa stempu kwa kazi hizo jambo ambalo limekuwa                likikiukwa na wafanyabiashara wanaosambaza na kuuza kazi                hizo hivyo kupelekea Serikali kuendesha operesheni ya                kusaka kazi za filamu na muziki zisisokuwa na haki miliki                na stempu kutoka TRA.
        Akitoa mchango wake                Katibu Mtendaji kutoka Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fisoo                amewataka wafanyabiashara wa kusambaza na kuuza kazi za                filamu na muziki zinazotoka nje ya nchi na za hapa nchini                kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kuweza kulinda                mali zao na kufanya biashara kwa amani.
        Bibi. Fisoo amesema kuwa                kifungu cha 19, 1 cha sheria ya haki miliki ya mwaka 1996                kimefafanua kuwa uuzaji, usambazaji, ukodishaji na                uonyeshaji wa filamu za picha jongevu uzingatie usajili                kutoka Bodi ya Filamu kuziwezesha kazi hizo kuwa halali                zinaposambazwa.
        Naye Afisa Mtendaji Mkuu                kutoka COSOTA Bibi. Doris Antony amewataka wafanyabiashara                kuheshimu haki miliki za wasanii kwani mmiliki wa kazi ya                filamu na muziki ana haki 9 ambapo kati ya haki hizo tisa                ni pamoja na haki ya kusambaza kazi yake, haki ya                kuzalisha, haki ya kutafsiri, haki ya kuonyesha kwa Umma,                haki ya kupeleka kwenye vyombo vya habari pamoja na haki                ya kupeleka nje ya nchi.
        Wakitoa mchango wao,                wanaumoja wa uingizaji na uuzaji wa kazi za filamu na                muziki zinazotoka nje ya nchi wameiomba serikali kuwapa                nafasi kumalizia mzigo uliopo sokoni kwa madai kuwa                hawakuwa na ufahamu wa sheria inayosimamia haki miliki                kitu ambacho serikali imekipinga na kuwataka kufuatilia                haki miliki ya kazi walizonazo kwa wamiliki kuiwezesha                serikali kutoa stempu zitakazowawezesha kuuza kazi hizo.
        

Comments
Post a Comment