USIKU WA MWANA DAR ES SALAM WAFANA …wasanii wa Extra Bongo wajilipua, wa Mashujaa Band wageuka njozi za mchana ...pata picha 20
HATIMAYE onyesho la Usiku wa Mwana Dar es Salaam limefanyika ndani ya ukumbi wa Mango Garden na kuhudhuriwa na mashabiki wengi lakini bado kiu ya kuwaona wanamuziki wote walioshiriki kuunda albam ya Mwana Dar es Salaam ikawa ni kitendawili kigumu.
Onyesho hilo ambalo kwa wiki kadhaa liliteka hisia za mashabiki wa muziki wa dansi na kupelekea kuwa na ubishani mkali mithili ya ule wa Simba na Yanga, umehitimisha kile ambacho Saluti5 ilikiita "Mbivu na Mbichi" na sasa karibu maswali yote magumu show hiyo, yamepata majibu.
Katika habari ya awali ya Saluti5 iliandika hivi: Yote kwa yote, maswali magumu yanabaki pale pale: "Je wanamuziki wa Mashujaa na Extra Bongo wataruhusiwa katika dakika za lala salama? Je wasiporuhusiwa watakaidi amri za waajiri wao? Je wakikaidi amri za waajiri wao nini itakuwa hatma yao? Je Twanga Pepeta watakuwa tayari kuwapandisha jukwaani wanamuziki hao licha ya karipio la waajiri wao?"
Baada ya onyesho hilo kukamilika, majibu yafuatayo yamepatikana. 1.Wanamuziki wa Extra Bongo na Mashujaa hawajaruhusiwa hadi dakika ya mwisho. 2.Wasanii watatu wa Extra Bongo wamekaidi amri ya mwajiri wao. 3.Wasanii wa Mashujaa Band wametii amri ya mwajiri wao na hakuna hata mmoja aliyepanda jukwaa la Usiku wa Mwana Dar es Salaam (ukiondoa Lilian Internet ambaye ni kama amejiungua kwenye bendi hiyo siku nyingi zilizopita). 4.Twanga Pepeta wakawapandisha jukwaani wasanii wa Extra Bongo waliojipua licha angalizo la kupoteza ajira zao kama ilivyotolewa na boss wa Extra Bongo Ally Chocky.
Wasanii wa Extra Bongo waliojilipua ni madansa Sabrina, Maria Soloma na Danger Boy.
Kwa kukosekana wasanii wa Mashujaa - Chaz Baba na Ferguson kukapelekea jumla ya washika vipaza sauti watatu walioshiriki kurekodi albam ya Mwana Dar es Salaam kukosekana, hii ni kutokana na kutokuwepo pia kwa mwimbaji wa kike Janet Isinika.
Khalid Chokoraa, Rogart Hegga, Amigolas na Msafiri Diouf ndio wasanii wa safu ya mbele (kutoka nje ya Twanga) waliokuwepo, lakini ni Chokoraa ndiye aliyeiteka show zaidi.
Chokoraa kutoka Mapacha Watatu alisisimua mashabiki wengi tangu alipoingia jukwaani kwa staili ya aina yake na ndiye msanii aliyetunzwa pesa nyingi zaidi kuliko yeyote yule.
Ukiachana na hayo, onyesho lililosindikizwa na TOT Band, lilikuwa tamu na kwa hakika liliwakumbusha watu mbali sana na kuwafanya watawaliwe na hisia kali.




















Comments
Post a Comment