Shaw Hassan Shaw



Shaw Hassan Shaw

Kwa wapenzi wa Vijana Jazz wanakumbuka vile vipande vya keyboards vilivyokuwa vikianzisha zile nyimbo mbili alizokuwa akiimba Kida Waziri, Penzi Haligawanyiki na Shingo feni, mpigaji wake alikuwa Shaw Hassan Shaw Rwamboh. Mwanamuziki huyu alizaliwa

tarehe 25/sept/1959, Dar Es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gitaa na wenzie kando ya Ziwa Tanganyika huko Kigoma, wakitumia magitaa ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi. Aliporudi Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gitaa kiasi cha kukubaliwa na Patrick Balisidya kupiga gitaa la rythm katika bendi yake ya pili PAMA Band, chini ya Afro70.

Ni chini ya malezi ya Patrick alipojifunza kupiga Keybords (Kinanda). Baada ya hapo aliacha muziki na kujiunga na Dar Technical College. Lakini 1980 alijiunga na Vijana Jazz kama mpiga Keyboards, alishirikiana na wanamuziki wengi lakini wengi pia wametangulia mbele ya haki. Waliobaki kati ya aliyokuwa nao wakati huo ni John Kitime, Abuu Semhando, Kida Waziri, Saad Ally Mnara, Hamisi Mirambo, Hassan Dalali, Hamza Kalala na Rashid Pembe. Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound, chini ya Maalim Muhidin Gurumo (MJOMBA), na Marehemu Abel Baltazar , hapa alikutana na wanamuziki kama Benno Villa Anthony na Mhina Panduka (Toto Tundu) .Aliacha bendi baada ya miezi sita tu, mwenyewe anasema, '….kutokana na muhusika kutozingatia mkataba wangu…'. Alihamia Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga Mawimbini Hotel, hakukaa sana kwani Washirika Tanzania Stars walimwita. Hapa akakutana na Zahir Ally, Ally Choki Rwambow, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, Abdul Salvador na wengine, ilitokea kutoelewana baina ya wanamuziki na yeye kama kiongozi wa bendi ilibidi aachie ngazi kuepusha bendi kuzidi kujichanganya. Baada ya hapo Kanku Kelly ambaye ni mume wa dada wa mke wake alimuita ajiunge na Kilimanjaro Connection Band. Anasema Kanku alimvumilia sana kwa kuwa alikuwa hajawahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani, pili hii bendi ilikua inazunguka kwa kupiga muziki hotel mbalimbali Malaysia,Singapore, Indonesia,Thailand na Japan jambo ambalo lilifanya aone kila kitu ni kigeni. Katika bendi hiyo alishirikiana na akina Kanku Kelly, Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan, Shomari Fabrice, Bob Sija, Fally Mbutu, Raysure boy,Delphin Mununga na Kinguti System. Baadaye Shaw, Kinguti na Burhan Muba waliamua kuanzisha kundi dogo wakitumia sequencer keyboards na kumuaga Kanku Kelly. Group hiyo ilijiita Jambo Survivors Band, itakumbukwa kwa ule wimbo Maprosoo uliokuwa katika album ya MAPROSOO. Baada ya hapo bendi ikaanza kuzunguka nchi mbalimbali ikipiga katika mahotelini. Wameshapita Oman , Fujairah, U.A.E, Singapore, Malaysia na sasa wapo Thailand. Shaw anasema wanamuziki ambao hatawasahau kwa kuwa wamemfikisha alipo ni Zahir Ally Zorro, Marehem Patrick Balisdya, Waziri Ally, Kinguti System, Burhan Muba na Kanku Kelly. Kituko ambacho hawezi kusahau ni nchini Malasyia akiwa na Kanku Kelly kwa mara ya kwanza kupiga muziki akiwa amezungukwa na watu weupe Anasema nyimbo zote zilipotea kichwani akawa hakumbuki hata nyimbo moja.

(Picha ya juu Burhan Muba, Kinguti System ,Hassan Shaw, ya chini ni Vijana Jazz, Hassan Shaw wa mwisho kulia)





Comments