PICHA 22: UZINDUZI WA ALBAM MPYA YA MASHAUZI CLASSIC BALAA! MANGO GARDEN YATAPIKA …Isha naye aacha gumzo
UZINDUZI wa albam mpya ya Mashauzi Classic "Asiyekujua Hakuthamini" uliofanyika Alhamisi usiku, umefana, umesisimua, umekosha, umefurahisha na kuacha gumzo la aina yake.
Ukumbi wa Mango Garden Kinondoni ambao ndio uliokuwa nyumba ya uzinduzi huo, ulijaa hadi kutapika huku burudani zote kuanzia zile za usindikizaji hadi uzinduzi wenyewe, zikiwapagawisha vilivyo mashabiki waliofurika ukumbini hapo.
Mkongwe Ally Star, Cassim Mganga na Ben Pol walifanya vema katika kusindikiza uzinduzi wa "Asiyekujua Hakuthamini" lakini mandhari ya ukumbi wa Mango Garden ikabadilika kabisa majira ya saa 6 za usiku pale mkurugenzi wa Mashauzi Classic, Isha Ramadhan alipoingia jukwaani kwa staili ya aina yake. (Katika habari itakayofuata baada yah ii, tutakusimulia namna Isha alivyoingia sambamba na mtiririko mzuri wa picha zitakazokupa sura kamili ya tukio hilo).
Kwa hakika lilikuwa ni onyesho bab kubwa na ilikuwa ni zawadi nzuri ya kufunga msimu wa kwanza wa burudani mwaka 2014 (kabla ya kuanza mfungo wa Ramadhan) – Hakukuwa na dosari yoyote hata kama ungeitafuta kwa tochi bado usingeiona – Mashauzi walijipanga vizuri.
Albam ya ASIYEKUJUA HAKUTHAMINI inaundwa na nyimbo tano: "Asiyekujua Hakuthamini" ulioimbwa na Isha na mdogo wake (Saida Ramadhan), "Bonge la Bwana" wa Hashim Said, "Ni Mapenzi tu" wa Zubeda Malick, "Ropokeni yanayowahusu" uimbaji wake Saida Ramdhan na "Wema Hauozi na Ubaya haulipizwi" wa Asia Mzinga.
Comments
Post a Comment