PICHA 20 ZA NAMNA ISHA ALIVYOINGIA JUKWAANI UZINDUZI WA ASIYEKUJUA HAKUTHAMINI …ilikuwa kama bonge la filamu …ukumbi watingwa taharuki, woga, lakini baadae furaha
ISHA Mashauzi aliingia kwenye uzinduzi wa albam mpya ya bendi yake ya Mashauzi Classic kwa staili ya aina yake iliyowaweka watu na kihoro mwanzo mwisho.
Uzinduzi wa albam hiyo "Asiyekujua Hakuthamini" ulifanyika Alhamisi usiku ndani ya ukumbi wa Mango Garden Kinondoni.
Kuna wakati watu walipigwa na mshangao, kisha furaha, mara taharuki, woga lakini baadae furaha ikarudi tena.
Wala watu hawakujua nini kilichokuwa kinaendelea pale walipoona wacheza kiduku na mabaunsa wamebeba pakacha kubwa lililokuwa na maembe na kuingia nalo ukumbini.
Wakalifikisha Pakacha lile jukwaani na kuanza kula maembe. Wakati watu bado wana shauku ya kujua kinachoendelea, Isha akaibuka kweye pakacha lile lenye maembe, mashabiki wakapagawa na kushangilia kwa kelele.
Lakini isha alikuwa hajamaliza. akajidondosha chini. Watu wakadhani amedondoka kwa kuzidiwa au kuugua ghafla …ukumbi ukakumbwa na taharuki.
Akiwa amevalia mavazi yaliyotengenezwa maalum kwaajili ya tukio hilo, kukawa na usanii wa hali ya juu umefanywa wa kufunga utumbo uliopikwa ndani ya mavazi yake.
Huku akiwa bado amelala chini kama mtu aliyezimia au kufariki, nguo zake zikaanza kuchanwa, wabebaji wale wa pakacha wakafanya kama wanampasua tumbo.
Kwa haraka haraka mtu angeweza kudhani Isha amepasuliwa kweli tumbo na ule unaoonekana ni utumbo wake halisi. Mashabiki wakaendelea kupingwa ganzi wasijue nini kinachoendelea.
Watu wale wakaanza kunyofoa utumbo na kuutafuna. Watu wakaendelea kupigwa na butwaa. Kisha kikavutwa kitambaa kwenye utumbo huo kikiwa kimeandikwa ASIYEKUJUA HAKUTHAMINI. Kikanyanyuliwa juu kuonyesha kuwa sasa uzinduzi rasmi unaanza.
Isha naye akainuliwa, akapozi kidogo shangwe zikatawala ukumbi mzima - akapiga show moja kisha ukafuata wimbo Asiyekujua Hakuthamini aliouimba na Saida Ramdhani.
Baadae Isha akaenda kubadili nguo na aliporejea jukwaani akawa ni Isha mwingine kabisa.
Kilichofuata baada ya hapo ni burudani juu ya burudani kutoka kwa kundi zima la Mashauzi Classic.
Comments
Post a Comment