Marijani Rajabu



Marijani Rajabu Marijani Rajabu kwa vyovyote ni mmoja wa wanamuziki ambao wametoa mchango mkubwa katika ulimwengu huu wa muziki. Japo ni miaka mingi toka mauti yake yalipomfika, bado nyimbo zake zinapigwa na wanamuziki mbalimbali majukwaani na hata kurudiwa kurekodiwa tena. Marijani alizaliwa maeneo ya Kariakoo mwaka 1954. Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji. Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia. Alilelewa vizuri kwa misingi ya dini ya Kiislam kwa hivyo alihudhuria mafunzo ya dini utotoni kama inavyotakiwa. Akiwa na umri wa miaka 18 hivi, alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii ilikuwa unajulikana kama The Jets. Katika bendi hii Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya Phillips. Mwaka 1972 Marijani alihamia bendi ya Safari Trippers. Hapa ndipo ubora wake ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Safari Trippers kuwa moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo na kuweza kuzunguka nchi nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake vizuri. Bendi wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati bendi ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo. Miezi michache baadae Marijani na wenzie waliibukia Dar International. Pia huku kulikuwa na wanamuziki wazuri na haraka bendi ilipata umaarufu wa hali ya juu kwa vibao vyake kama Zuena na Mwanameka. kutokana na hali wakati huo bendi ilirekodi vibao hivi RTD na kuambulia sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao. Kati ya mwaka 1979 na 1986 bendi ilipiga karibu kila wilaya nchi hii na kufurahisha sana watu na mtindo wao wa Super Bomboka. Uchakavu wa vyombo hatimae mwaka huo 1986, ukamaliza mbio za bendi hii. Kwa miezi michache Marijani akashiriki katika lile kundi kubwa la wanamuziki 57 waliotengeneza Tanzania All Stars, kundi hili lilirekodi vibao vinne ambavyo si rahisi kwa bendi zilizopo sasa kufikia ubora wake kimuziki. Marijani alipitia Mwenge Jazz kw muda mfupi, na kukaa kama mwaka mmoja Kurugenzi Jazz ya Arusha, kisha akajaribu kuanzisha kundi lake la Africulture na mtindo wa Mahepe lakini kwa ukosefu wa vyombo mambo hayakuwa mazuri. Kufiki1992 hali ya Marijani ilikuwa ngumu akiishi kwa kuuza kanda zake ili aweze kuishi.Pamoja na nyimbo nyingi, za kuimbia Chama tawala na serikali, na hata tungo yake Mwanameka kutumiwa katika mtihani wa kidato cha Nne. Rajabu Marijani hajawahi kukumbukwa rasmi kama mmoja wa wasanii bora Afrika ya Mashariki

Comments