HII NDIYO KAULI YA DANGER BOY ALIYETIMULIWA EXTRA BONGO …Maria Soloma naye atoa dukuduku lake



HII NDIYO KAULI YA DANGER BOY ALIYETIMULIWA EXTRA BONGO …Maria Soloma naye atoa dukuduku lake
HII NDIYO KAULI YA DANGER BOY ALIYETIMULIWA EXTRA BONGO            …Maria Soloma naye atoa dukuduku lake

DANSA wa kiume aliyetimuliwa Extra Bongo, Danger Boy (kushoto pichani) ameongea na Saluti5 na kufafanua juu ya yaliyomsibu kwa kushiriki kwake onyesho la Mwana Dar es Salaam.

Danger Boy ni mmoja wa wasanii watatu wa Extra Bongo waliokumbwa na panga baada ya kushiriki Mwana Dar es Salaam kinyume na amri iliyotolewa na uongozi wa Extra Bongo.

Danger Boy ameongelea mambo manne: 1.Kufukuzwa, 2.Kwanini alishiriki Mwana Dar es Salaam, 3. Madai ya kushiriki tamasha kwa sababu hawajalipwa mshahara, 4. Uwezekano wa kurejea Extra Bongo iwapo Chocky atabadili maamuzi yake.

1. KUFUKUZWA:

"Namheshimu sana Ally Chocky, ni mkurugenzi wangu, ni boss wangu, ana mchango mkubwa kwangu na bendi yake pia ina mchango mkubwa kwangu, nimekaa pale kwa muda mrefu .

"Kama ameamua hivyo sina njia nyingine ya kufanya zaidi ya kukubali matokeo na kuangalia kitu kingine cha kufanya".

KWANINI ALISHIRIKI MWANA DAR ES SALAAM?

"Nilishawishika kushiriki Mwana Dar es Salaam si kwa kingine bali ni wanamuziki ambao nimewahi kufanya nao kazi, nilihamasika kukutana na watu ambao sijakaa nao jukwaa moja kwa miaka mingi.

"Wakati nashiriki onyesho hilo sikuwa nimedhamiria kuwa sasa naondoka Extra Bongo. Niliamini kuwa Chocky kama mkurugenzi wangu nitaongea nae na kumuomba radhi na atanielewa."

MADAI YA KUSHIRIKI TAMASHA KWASABABU HAWAJALIPWA MISHAHARA:

"Kiukweli kabisa, mimi binafsi sijashiriki tamasha kwasababu ya mishahara."

JE YUPO TAYARI KUREJEA EXTRA BONGO KAMA CHOCKY ATABADILI MAAMUZI?

"Extra Bongo ndiyo nyumbani kwangu, ndiyo kazini kwangu. Mimi kama Chocky ataniambia yameisha rudi tufanye kazi, tunafanya kazi, sina tatizo.

"Kama ningetaka kuondoka Extra Bongo ningefuata taratibu za kuondoka lakini sio kwa kushiriki Mwana Dar es Salaam, hapana kabisa."

Hayo ndiyo maneno ya Danger Boy. 

Wakati Danger akiyasema hayo, dansa wa kike Maria Soloma (pichani kulia) ambaye naye pia ametimuliwa Extra Bongo kwa kosa hilo hilo, amedai hakuna kinachomshtua kwa vile alikuwa tayari kwa lolote.

Maria alikuwa na haya ya kusema: "Nilipoamua kushiriki onyesho lile nilishakata shauri kupokea maamuzi yoyote yale.

"Mimi niliingia Extra Bongo kwa mkataba ambao uliisha tangu tarehe 8 mwezi huu kwahiyo nilikuwa huru kushiriki onyesho la Mwana Dar es Salaam.

 "Niliendelea kuwepo Extra Bongo kwa kuamini kuwa tungefikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya hasa kuwa kuzingatia kuwa nina haki zangu nyingi ambazo nadai katika mkataba ulioisha.

"Kama Chocky ameamua kunifukuza sio hatari ila ni vizuri akanilipa haki zangu ninazomdai ambazo kwa muda huu sipendi kuziweka wazi."

Saluti5 bado haijafanikiwa kumpata Sabrina, dansa mwingine aliyetimuliwa Extra Bongo.



Comments