HATIMAYE YAMETIMIA: CHOCKY ATIMUA WOTE WALIOSHIRIKI USIKU WA MWANA DAR ES SALAAM …azungumzia pia suala la mishahara
MKURUGENZI wa Extra Bongo amewatimua wasanii wake watatu walioshiriki tamasha la Usiku wa Mwana Dar es Salaam.
Akiongea na Saluti5 jana usiku, Ally Chocky alisema msimamo wake hauyumbi na kwamba wasanii hao wamejifukuzisha wenyewe.
"Yuko mmoja tayari kaleta barua ya kuomba msamaha lakini hilo halisaidii, waendelee na ushujaa wao, hakuna nafasi tena ya wao kupokelewa Extra Bongo," alisema Chocky.
Wasanii walioshiriki Usiku wa Mwana Dar es Salaam uliofanyika Mango Garden Jumamosi iliyopita, ni Danger Boy, Sabrina na Maria Soloma.
Sabrina
Danger Boy na Maria Soloma
Chocky amesema ameshangazwa sana na dansa mmoja kati ya hao ambaye amekuwa akitangaza kuwa Extra Bongo hailipi mshahara na wakati huo huo yeye ndiye amekuwa wa kwanza kuandika barua ya kuomba msamaha.
Ally Chocky amewataka wasanii na viongozi wa bendi wasitumie kigezo cha kutolipwa mshahara kama fimbo ya kuvunja sheria.
"Hivi ni bendi gani ambayo haidaiwi mshahara japo na msanii wake mmoja?" anahoji Chocky.
"Ziko bendi ambazo zimepoteza kabisa uwezo wa kulipa mishahara kwa wasanii wake wote na kuishia kulipa posho tu za maonyesho ambazo nazo ukitajiwa ni kituko," aliongeza Chocky.
Mkurugenzi huyo wa Extra Bongo amewataka wasanii wenye tabia ya kutangaza kucheleweshewa mishahara, wawe pia wepesi wa kutangaza pale wanapolipwa mapema mishahara yao.
"Ugumu wa bishara ya muziki wa dansi unajulikana, bendi nyingi zinashindwa kujiendesha kwa kipato kinachopatikana ukumbini, hivyo wakati mwingine suala la kuchelewa kwa mishahara halikwepeki," alifafanua Ally Chocky.
Aidha, Chocky ameendelea kusisitiza kuwa onyesho la Mwana Dar es Salaam lililenga kuzalisha mgogoro baina ya wamiliki wa bendi na wasanii ili watu wajizolee wasanii wa bure pale watakapotimuliwa na bendi zao.
"Ukitaka kuthibitisha hilo subiri uone wasanii hao watajiunga na bendi gani," alimaliza Chocky.
Comments
Post a Comment