ALIYEKUWA kocha wa Manchester United David Moyes ameahidiwa kitita cha pauni milioni 4 kwa mwaka ili kumrithi Roberto Mancini kama kocha wa Galatasaray ya Uturuki.
Iwapo mkataba huo utakubaliwa na ''The Chosen one'' huenda raia huyo wa Scotland akarejea katika safu ya ukufunzi miezi michache tangu atimuliwe huko Old Trafford kufuatia msururu wa matokeo duni.
Kibarua chake kiliota nyasi huko Old Trafford mwezi Aprili Manchester ikiwa katika nafasi ya saba katika ligi ya Uingereza msimu mmoja tu tangu watwae ubingwa chini ya mkufunzi shupavu Sir Alex Fergusson.
Galatasaray imedhibitishia waandishi wa habari kuwa Moyes alizuru Istanbul ili kufanya mkutano na rais wa klabu hiyo Unal Aysal.
Galatasaray, ilimaliza katika nafasi ya pili msimu uliokwisha nyuma ya Fenerbahce japo mabingwa hao wamepigwa marufuku ya kushiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa udanganyifu katika baadhi ya mechi zao.
Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa vigogo hao wa ligi ya Uturuki Kufunzwa na Muingereza, mwaka wa 1995 waliwahi kufunzwa na kocha Graeme Souness.
Comments
Post a Comment