AVEVA: Nipeni Simba Niinyooshe Yanga



AVEVA: Nipeni Simba Niinyooshe Yanga
WANACHAMA wa klabu ya Simba Jumapili ya wiki hii watachagua viongozi wapya wa klabu hiyo katika ngazi ya urais, makamu wa rais na wajumbe wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo watakaopewa dhamana ya uongozi kwa miaka minne ijayo.

Mmoja wa wagombea urais wa klabu hiyo, Evans Aveva alizungumza na Mwanaspoti na kutoa sera zake endapo atafanikiwa kuingia madarakani.

"Sera yangu kuu ni kuleta umoja ndani ya klabu ya Simba, sitaki kuona Mwanasimba anajitofautisha na mwenzake kisa ametoka kwenye kundi fulani, sisi sote nia yetu ni moja hivyo nitajitahidi kwenye uongozi wangu kuhakikisha tunakuwa na umoja.

"Sera yangu ya pili ni kutaka Simba icheze mpira, tumedhalilika sana, wapenzi wa klabu yetu wamefedheheshwa sana na matokeo mabovu ya klabu yetu hivyo mimi nimepanga kurejesha heshima hiyo, nataka klabu yetu icheze soka safi na la kisasa.

"Katika kulifanikisha hilo nitahakikisha kuwa nafanya usajili wa kikosi imara, wachezaji wanakuwa na mazingira mazuri ya kazi, naboresha mishahara yao na masilahi yao mengine ili waweze kuweka akili yao kwenye mchezo," anasema Aveva.

"Nitaangalia wachezaji wazawa zaidi kwa sasa, kwa wachezaji wa kimataifa nitahakikisha tumefanya skauti za maana ili kuepuka kusajili wachezaji wenye uwezo wa chini, tunataka kuhakikisha Simba inakuwa na wachezaji wenye hadhi ya kucheza kwenye klabu yetu na siyo kuokota okota tu."

"Mbali na hilo nitaziunganisha kamati ya usajili na ile ya ufundi, tunatakiwa tuwe na taasisi moja kubwa ambayo itatuletea wachezaji wa maana, nimepanga kuona wanakuwa na maskauti wa usajili wa ndani na nje ya nchi, wa ndani watatazama mechi zote za Ligi Kuu na kutuletea mapendekezo ya maana."

Kuongeza pato la klabu

"Kwa sasa tunashindwa hata kuuza jezi za klabu yetu kutokana na mwenendo mbovu wa timu, nitaweka nguvu kubwa kwenye heshima ya soka uwanjani na hiyo ndiyo itasaidia kukuza kipato chetu.

"Watu wataingia kwa wingi kuitazama Simba, watu watanunua jezi za Simba, pia nitajitahidi kushirikiana na viongozi wenzangu kuona namna ya kuanzisha bidhaa nyingine za klabu kama vile vikombe, kalamu skafu na kadhalika," anasema Aveva.

"Kikubwa ninachoamini ni kuwa kuiwezesha Simba kucheza mpira, wadhamini watakuja wenyewe tu, kwa mfano mpaka sasa wadhamini watatu wameonyesha nia ya kuingia udhamini na sisi iwapo nitaingia madarakani, wameonyesha kuniamini hivyo tukicheza kwa kiwango cha juu itakuwa zaidi ya hapo."

Aveva anaongeza kuwa atahakikisha kuwa idara ya masoko atayaoiunda itasimamia na kukuza mauzo ya bidhaa za klabu hiyo pamoja na kubuni njia nyingine za mapato za klabu hiyo ikiwemo namna ya kuboresha jengo la klabu hiyo lililopo eneo la Kariakoo, Dar es Salam.

Comments