PAUNI MIL 8 TU KUMPELEKA LOIC REMY ARSENAL AU LIVERPOOL …kipengele cha mkataba wake QPR chamkata maini kocha Redknapp
KOCHA wa QPR, Harry Redknapp anaamini mshambuliaji wake Loic Remy ataondoka msimu huu kutokana na utashi wake wa kucheza Ligi ya Mabingwa.
Redknap amefichua kuwa nyota huyo wa Ufaransa ana kipengele kinachomruhusu kuondoka QPR kwa pauni milioni 8.
Hali hiyo inatarajiwa kuamsha vita vikali kati ya Liverpool na Arsenal ambazo zote kwa pamoja zimeonyesha nia ya kupata huduma ya Remy aliyekipiga kwa mkopo Newcastle msimu ulioisha.
Alikuwa na msimu mzuri baada ya kutupia wavuni mabao 14 katika mechi 24 alizoanza – lakini pamoja na hayo, hajaonyesha nia ya kuwa na mkataba wa kudumu Newcastle.
QPR imerejea Ligi Kuu Jumamosi iliyopita baada ya kuinyuka Derby County 1-0 katika fainali iliyopigwa uwanja wa Wembley.
Licha ya kupanda daraja, Redknapp anaamini njozi ya kucheza Ligi ya Mabingwa itamuondoa Remy QPR.
Inaaminika kuwa, tayari Liverpool na Arsenal wameanzisha maongezi na mshambuliaji huyo, lakini mwenyewe angependa kusubiri hadi baada ya michuano ya Kombe la Dunia ndio aamue hatma yake.
Remy mwenye umri wa miaka 27, alijiunga na QPR Januari 2013 akitokea Marseille.
Comments
Post a Comment