MISAMBANO BALAA TUPU! AMWAGA TAMBO ZA HATARI ITV …asema anastahili tuzo ya heshima, adai yeye ndiye kafanya watu wa Masaki wapende taarab, atamba hakuna bendi isiyoijua Asu
MWIMBAJI wa taarab Abdul Misambano ametamba kuwa anastahili tuzo ya heshima inayotolewa na Kilimanjaro Tanzania Music Awards kwa vile yeye ni kioo cha waimbaji wa kiume waliopo hivi sasa.
Akiongea na ITV kupitia kipindi cha Shamsham za Pwani kinachotangazwa na Hawa Hassan, Misambano alidai waimbaji wengi wameanzia kuimba wimbo wa Asu kabla hawajawa waimbaji kamili.
Misambano alisema: "Karibu kila mwimbaji ninaekutana nae ananiambia alianzia kwenye wimbo wa Asu.
"Fanya utafiti, utagundua hakuna bendi hata moja ya taarab isiyoijua Asu, kuanzia za vichochoroni hadi bendi kubwa.
"Kila onyesho ninalokaribishwa katika bendi yoyote lazima watanipigia aidha "Asu" au "Utapendaje wawili". Mimi huwa siimbi wimbo wa mtu.
"Asu nimeitoa mwaka 1997 wakati wote wanaoimba sasa hivi walikuwa bado hawajawa wanamuziki, pengine hata Mzee Yusuf wakati huo bado alikuwa si mwanamuziki, lakini wote hao wanaupiga Asu, jiulize wameujuaje? Ni kwamba walikuwa wanausikia na wakaukubali.
"Ukiondoa Ally Star, waimbaji wengine wote wa kiume wanaoimba kwenye mabendi ya taarab wamenikuta kwenye game.
"Mimi mimi nikijihesabu ni msanii pekee Tanzani hii niliyesababisha taarab iingie Masaki iingie Upanga. Nastahili tuzo, wanipe wasisubiri hadi nife."
Misambambo pia alitamba kuwa nyimbo zake mpya atakazotoa mwaka huu zitakuwa moto wa kuotea mbali na kwamba lazima zimpeleke tuzo za Kili mwaka ujao.
"Nina ladha ya peke yangu halafu najua mashabiki wangu wanataka nini," alitamba Misambano.
Msikilize Misambano hapo chini upate tambo zake kwa mapana zaidi.
Comments
Post a Comment