Mashindano ya Mchezo wa Safari Lager National Pool Championship 2014 yazinduliwa leo jijini Dar




Mashindano ya Mchezo wa Safari Lager National Pool Championship 2014 yazinduliwa leo jijini Dar
MASHINDANO ya mchezo wa pool ya 'Safari Lager National Pool Championship 2014', ngazi ya mikoa yanatarajia kuanza Juni 14, mwaka huu katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa Chama cha Mchezo huo Taifa (TAPA), Amosi Kafwinga amesema mashindano hayo ambayo kwa ngazi ya taifa yatamalizika mwezi Septemba 14, mwaka huu.

Kafwinga amesema fainali za taifa za mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania(TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager, ambayo yatashirikisha mabingwa wa kila mkoa, yatafanyikia mkoani Kilimanjaro September 14 .

Aliongeza kwa kuitaja mikoa itakayoshiriki mashindano hayo kuwa ni pamoja na mikoa maalum ya kimichezo ya Kinondoni, Ilala, Temeke, Pwani, Marogoro, Dodoma, Tanga, Lindi, Manyara, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Kagera na Iringa.

Naye Meneja wa bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo amesema jumla ya Sh.Mil.86 zimetengwa kwa ajili ya mashindano hayo ikiwa imeongezeka kwa asilimia 15 ikilinganisha na bajeti ya msimu uliopita.

Shelukindo amesema wameamua kuboreshwa kwa zawadi za washindi ni kuongeza changamoto zaidi kwa klabu zitakazoshiriki mashindano hayo. Alisema bingwa wa kila mkoa kwa upande wa timu atapata Sh.800,000 kutoka Sh.500,000 ya msimu uliopita, mshindi wa pili Sh.400,000, mshindi wa tatu Sh.250,000.

Shelukindo amesema kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume), bingwa atapata Sh.400,000, mshindi wa pili Sh.250,000, wakati bingwa kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanawake), atapewa Sh.300,000 na mshindi wa pili Sh.200,000. Alisema bingwa wa fainali za taifa kwa pande wa klabu ataondoka na fedha taslim Sh.Mil.5
Meneja wa Bia ya Safari Lager,Oscar Shelukindo (kulia) akikabidhi Kombe litakalokabidhiwa kwa Bingwa wa Mchezo wa Pool Taifa 2014,Kwa Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa Pool Taifa (TAPA),Isack Togocho (kushoto) mara baada ya uzinduzi rasmi wa mashindano hayo uliofanyika leo kwenye Ukumbi wa Safari Pub,Ilala Mchikichini jijini Dar es Salaam.Katikati ni Katibu Mkuu wa TAPA,Amos Kafwinga. 
Meneja wa Bia ya Safari Lager,Oscar Shelukindo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi rasmi wa mashindano mchezo wa Pool kwa ngazi ya mikoa mpaka Taifa uliofanyika leo kwenye Ukumbi wa Safari Pub,Ilala Mchikichini jijini Dar es Salaam.Kulia ni Katibu Mkuu wa TAPA,Amos Kafwinga.
Uzinduzi rasmi ukifanyika kwa kucheza mchezo huo.


Comments