LICHA YA BARCELONA KUSEMA HAUZWI, FABREGAS AOMBA UHAMISHO …Man United na Arsenal zawekwa mkao wa kula
MIAMBA ya England Arsenal na Manchester United wamewekwa mkao wa kula kwa mara nyingine tena kufuatia ripoti kuwa Cecs Fabregas ATAONDOKA Barcelona kiangazi hiki.
Hapo jana ilidaiwa kuwa Fabregas hauzwi na kwamba wakali hao wa Catalan wamedhamiria kumbakisha klabuni nyota huyo mwenye umri wa miaka 27.
Hata hivyo ripoti mpya kabisa zinasema mwanasoka huyo wa zamani wa Arsenal ameomba uhamisho huku akiwa anataka kurejea tena Ligi Kuu ya England.
Inaonekana kituo chake kijacho kitakuwa aidha Manchester United ambayo ilijaribu kumsajili msimu uliopita au Arsenal iliyomuuza mwaka 2011 baada ya kuwa nae kwa miaka nane na kucheza zaidi ya mechi 200 pamoja na unahodha wa misimu mitatu.
Thamani ya Fabregas inatajwa kuwa ni pauni milioni 30 ingawa usajili wa David Luiz kwenda PSG kwa pauni milioni 50 na ule unaotarajiwa wa Adam Lallana kwenda Liverpool kwa pauni milioni 25, unaweza ukaongeza bei ya Fabregas.
Comments
Post a Comment