Haondoki Mchezaji Mbeya City, Simba na Yanga Mlie tu




Haondoki Mchezaji Mbeya City, Simba na Yanga Mlie tu
MBEYA City iliyoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kushika nafasi ya tatu, imesema haitajisahau kama ilivyokuwa kwa Tukuyu Stars iliyopanda daraja na kutwaa ubingwa mwaka 1986.

Mwaka huo Tukuyu Stars ilipanda daraja hadi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) na ikatwaa ubingwa, lakini msimu uliofuata ikaporomoka na kushuka.

Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, ambaye kwa sasa timu yake ipo Sudan ikishiriki mashindano ya Cecafa Nile Basin, alisema: "Tunajua kuwa kuna timu zinataka kutubomoa kwa kusajili wachezaji wetu, hatukatai kama kanuni zitafuatwa.

"Lakini tumeweka mikakati sahihi ya kuona hatupotezi mchezaji na wala hatutoki katika ubora wetu."

Kimbe alisema wachezaji wao wengi bado wana mikataba isiyopungua mwaka mmoja, hivyo klabu zinazowahitaji wachezaji wao zinapaswa kuwasiliana kwanza na uongozi wao ili wapewe mwongozo wa kufanya manunuzi.

Wachezaji wa Mbeya City wanaowaniwa na timu nyingine hasa Simba ni Saad Kipanga na Deus Kaseke ambao wanamudu kucheza nafasi za ushambuliaji na winga.

Katika hatua nyingine, Mbeya City, imemnyakua mchezaji mahiri wa timu ya Kata Kambasegela FC ya Busokelo, Philipo Mwalyaje (20) na kumchomeka kwenye timu ya vijana.

Mwalyaje ambaye ni mrefu mwenye unene wa kati, anacheza namba zote za ulinzi. Katibu Mkuu wa Kambasegela, Emmanuel Swila, alisema kijana wao alichukuliwa Mei 14 baada ya viongozi wa Mbeya City kumwona akisakata kambumbu kwenye mashindano ya Gwatengile yaliyoshirikisha timu nane ambapo timu yao iliibuka bingwa.


Comments