AUDIO: MIRINDA NYEUSI ATUMA SALAM TWANGA PEPETA …amtaka Asha Baraka awe mkweli, aomba rap zake mpya zisitumiwe



AUDIO: MIRINDA NYEUSI ATUMA SALAM TWANGA PEPETA …amtaka Asha Baraka awe mkweli, aomba rap zake mpya zisitumiwe
AUDIO: MIRINDA NYEUSI ATUMA SALAM TWANGA PEPETA …amtaka            Asha Baraka awe mkweli, aomba rap zake mpya zisitumiwe

JANA mchana rapa aliyetangazwa kuenguliwa Twanga Pepeta, Mirinda Nyeusi (pichani), alifika ofisi za Saluti5 na kutoa ufafanuzi wake juu ya taarifa ya Asha Baraka iliyotolewa na mtandao huu siku ya Jumamosi.

Mirinda anadai hakupunguzwa kazi Twanga Pepeta bali ni yeye aliyejiengua kundini zaidi ya wiki tatu zilizopita.

Rapa huyo alisema: "Nimejiengua siku nyingi, zaidi ya wiki tatu – nikakaa kimya kwasababu sikutaka malumbano, lakini Asha Baraka anajua ukweli ni kwanini nimejiengua.

"Pengine amehofia labda nitamsema vibaya akaamua kuniwahi kwenye mtandao, sijapenda hili jambo, Asha Baraka ni mwislamu awe mkweli.

Mirinda akongeza kwa kusema: "Suala la kuambiwa naimba vibaya Kiswahili ni majungu. Ni kweli nikiongea naongea kwa lafudhi ya Kikongo, lakini kwenye kuimba sina lafudhi hiyo kwasababu nasoma vizuri mistari na kukariri kichwani. Mbona Bella ni Mkongo lakini anaimba Kiswahili vizuri, mbona Wakongo wengi hapa wanaimba Kiswahili vizuri.

"Nimekuja hapa toka Vibration Sound na tangu kipindi hicho nimekuwa nikirekodi nyimbo za kiswahili. Twanga Pepeta nimetunga wimbo "Ngumu Kumeza" na unakubalika sana, kila ukianza kupigwa watu wote wanainuka, mbona hawakusema kiswahili kibovu?"

Mwisho kabisa Mirinda Nyeusi akamalizia kwa kuwataka Twanga Pepeta wafute rap zake kwenye wimbo mpya ambao bado uko studio.

"Nina rap mbili katika katika wimbo ule "Mpenzi utaniua na Presha" na "Heshima Pesa" naomba wazifute na wasimpe msanii mwingine azitumie. Waliobaki ni wasanii bora zaidi kwahiyo watunge vitu vyao.

"Nimesikia wanataka kuondoa sauti yangu halafu wampe mtu mwingine, tutafikishana pabaya, ile ni haki yangu na ni biashara.

"Kama Asha Baraka anataka kuzitumia aje tuongee biashara nimuuzie," alimaliza Mirinda ambaye alisema anamheshimu Asha Baraka na kwamba hataki kulumbana nae.

Sikiliza hapo chini sauti ya Mirinda Nyeusi akiongea kwa mapana zaidi, utaskia pia anavyorap vipande vitamu vya Presha na Heshima Pesa.



Comments