AUDIO: BANZA NDO BASI TENA EXTRA BONGO, MSIKILIZE CHOCKY AKISEMA AMENAWA MIKONO … asema yuko huru kujiunga na bendi yoyote
MKURUGENZI na mwimbaji wa Extra Bongo, Ally Chocky amesema bendi yake imenawa mikono kwa Banza Stone (pichani juu) na kusema kuanzia sasa si msanii wao tena.
Akiongea na Saluti5, Chocky alisema Banza amejiondoa mwenyewe na hivyo hawana kizuizi na maamuzi yake zaidi ya kukubaliana naye kwa vile ni mtu mzima na anajua analotenda.
Chocky anadai uongozi wa Extra Bongo umekwenda hadi kwa wazee wa Banza Stone na kuwasilisha maamuzi ya mtoto wao na wakawaelewa.
"Hii si mara ya kwanza kwa Banza kuacha bendi kienyeji, mara ya kwanza alifanya hivyo katikati ya mwaka jana," anasimulia Chocky.
Ally Chocky anafafanua zaidi: "Katika kipindi hicho Banza hakuonekana kazini kwa zaidi ya miezi mitatu bila taarifa yoyote na alipoulizwa akasema ameamua kupumzika, baadae akaanza kuugua, Extra Bongo tukaingia kwenye lawama – tukaambiwa tumetupa Banza. Watu wakasahau kuwa alishaacha bendi.
"Lakini hata hivyo hatukuwa tumemtupa Banza, tulishiriki katika kumuuguza, alivyopona tukamkaribisha tena kundini. Alirejea huku tukiamini atakuwa amebadilika kitabia.
"Hata hivyo tabia ya Banza haikubadilika akawa mgumu kufuata miiko ya kazi na hata miiko aliyopewa na daktari.
"Banza ameiacha bendi kwa mara nyingine tena, kwahiyo natangaza rasmi kuwa Banza hatuko naye tena, tumekabidhi kwa wazee wake na yuko huru kujiunga na bendi yoyote."
Msikilize Chocky hapo chini akizungumzia sakata la Banza
Comments
Post a Comment