MKURUGENZI wa Aset inayomiliki bendi ya The African Stars Band "Twanga Pepeta", Asha Baraka amemuengua rasmi kundini rapa Ibrahim maarufu kama Mirinda Nyeusi (pichani juu). Mwishoni mwa habari hii utaisikia sauti ya Asha Baraka kama ilivyorekodiwa na Saluti5.
Katika maongezi yake mahususi na Saluti5 Alhamisi jioni, Asha Baraka alisema Mirinda Nyeusi ameshindwa kuendana na mfumo wa Twanga Pepeta huku kiswahili chake kibovu nacho kikiwa pia ni moja ya sababu.
Mbali na Mirinda Nyeusi, Asha Baraka pia amesema bendi yake imemuondoa kundini mpiga solo Amos siku kadhaa zilizopita.
Wasanii wote hao wawili waliingia Twanga Pepeta mwaka jana baada ya kupunguzwa Mashujaa Band.
Asha Baraka alisema: "Mirinda Nyeusi ameshindwa kukubali ushauri wangu, nilimwambia awe na program maalum ya nyimbo zake za kikongo na si kuimba nyimbo za Twanga ambazo hajashiriki kurekodi.
"Anataka kuimba nyimbo za Banza au Amigo, kurap sehemu za Chocky, Chokoraa au Ferguson jambo ambalo badala ya kupendezesha nyimbo anakuwa anaziharibu.
"Ni mwanamuziki mzuri lakini hana uwezo wa kumkopi Banza, Chocky, Chokoraa, Ferguson wala Amigo, wapo wanaoweza lakini sio yeye.
"Ameshindwa kukuza matumizi yake ya lugha ya Kiswahili na hivyo nadhani anahitaji kwenda Malaika Band, Akudo au FM ambako wataoana zaidi lugha."
Akimzungumzia Amos, Asha Baraka alisema naye pia ameshindwa kuendena na mfumo wa Twanga. "Arudi zake Mashujaa, naskia wana matatizo ya mpiga solo," aliongeza Asha Baraka.
Asha Baraka ameongea mambo mengi na Saluti5 ambayo tutakuwa tukikuwekea moja moja kila siku.
Kwa leo hebu msikilize hapo chini anavyoongelea swala la Mirinda Nyeusi na Amos.
Comments
Post a Comment