YANGA O, SIMBA O … WANA WA JANGWANI WATUMIA PENGO LA MKUDE MANYIKA PETER JR AWABEBA MSIMBAZI …Canavarro ajitoa muhanga, Okwi presha tupu
Na Said Mdoe
MARA mpira ulipomalizika, makipa wote wa akiba wa Simba na Yanga – Ivon Mapunda na Juma Kasema wanaingia uwanjani na kwenda kumpongeza kipa wa Simba Peter Manyika Jr.
Wanamkubatia na kumgonga gonga mgongoni kuonyesha ishara ya kuikubali kazi kazi yake aliyoifanya langoni mwake.
Hiyo ilikuwa ni katika mchezo wa Ligi Kuu uliowakutanisha watani wa jadi – Simba na Yanga, ngoma iliyomalizika kwa sare ya bila kufungana.
Peter Manyika Jr ambaye ni mtoto wa kipa wa zamani wa Yanga Peter Manyika, ndiye aliyeibuka shujaa wa mchezo huo baada ya kuinyima Yanga nafasi kadhaa ambazo zingeweza kuzaa mabao ukingoni mwa mchezo.
Simba walicheza vizuri kipindi cha kwanza na kutengeza nafasi kadhaa, wakaendelea hivyo hadi mwanzoni mwa kipindi cha pili, lakini sura ya mchezo ikabadilika baada ya kiungo tegemeo wa Simba Jonas Mkude kutolewa baada kuumia nafasi yake ikachukuliwa na Pierre Kwizera.
Kuanzia hapo Yanga wakachanua, wakaanza gonga zenye macho zikiwemo zile za visigino, wakatengeneza mashambulizi yaliyofanya lango la Simba liwe hatarini na hapo ndipo ushujaa wa kipa chipukizi Peter Manyika Jr. uliponekana huku huu ukiwa ni mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu.
Beki na nahodha wa Yanga Nadir Haroub Cannavaro anabeba sifa nyingi kwa kujitoa muhanga kwa kucheza na mauvivu ya jeraha la jirani na jicho, akalilinda lango lake kwa kadri ya uwezo wake wakati kwa upande wa Simba, mshambuliaji Emannuel Okwi akiipa presha Yanga kwa muda wote wa mchezo.
Comments
Post a Comment